ZANZIBAR UNYANYASAJI AKINA MAMA NA WATOTO SASA BASI. - Mazengo360

Breaking

Saturday, 26 August 2017

ZANZIBAR UNYANYASAJI AKINA MAMA NA WATOTO SASA BASI.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imezindua mpango kazi wa miaka mitano wa kudhibiti vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto ambapo umelenga kurejesha hadhi na heshima ya mwanamke na mtoto katika jamii.

Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe Mandline Cyrus Castico akisoma kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein, taarifa  ya uzinduzi wa mpango wa serikali wa miaka mitano wa kudhibiti vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto mjini Zanzibar hivi leo.

Akizindua mpango huo leo mjini Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Mhe Dkt Ali Mohamed  Shein, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe Maudline Cyrus Castico  amesema, Serikali  imezindua mpango huo kwa kuwa inathamini utu wa raia wa Zanzibar.
Waziri Maudline alieleza pia kwamba, mpango huo umeweka  mikakati imara na madhubuti ya  kudhibiti vitendo vyote vya kikatili na vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto mfano kupigwa, kudhalilishwa kingono, kubakwa kwa wanawake na watoto na mengine yanayofanana na hayo, alieleza zaidi Mhe Waziri Mandline.
Pia, serikali imetoa rai kwa vyombo vyote husika katika mpango huu likiwemo jeshila polisi kushirikiana kwa pamoja ili kutekeleza mpango huo ili azma iliyokusudiwa na serikali itimie.
Akisoma risala yenye ujumbe toka kwa watoto wa Zanzibar mtoto Jaffar Ahmad alisema kupitia risala hiyo, vitendo  vya ukatili na udhalilishaji wanavyofanyiwa na jamiii inayowazunguka vimekuwa vikiwaumiza kisaikolojia na kuwarudisha nyuma katika masomo na hata kusababisha wasifurahie haki yao kama watoto katika jamii.
Risala hiyo pia ilibainisha wazi aina ya vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watoto, vikiwemo kupigwa, kulawitiwa, kuchomwa moto baadhi ya sehemu za viungo vya mwili pamoja na vichanga kutupwa ovyo kama mizoga, risala yao ilifafanua hayo.
Aidha watoto imeiomba  serikali kushirikiana na mashirika ya kimataifa pamoja na wadau wengine wa haki za binadamu pamoja na wale wa  maendeleo  hapa nchini,  ili kusimamia na kuwachukulia hatua madhubuti  wale wote watakaobainika kuendeleza vitendo vya udhalilishaji na kisha kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Nae Fatma Abdalla Mussa  akisoma risala ya wanawake wa Zanzibar ameitaka serikali kuyafanyia kazi na kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya udhalilishaji yanayowakumba   wanawake wa jamii ya Zanzibar.
Ujumbe huo wa wanawake pia umebainisha baadhi ya vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa vikiwemo kutelekezwa wao na watoto majumbani na waume zao.
Wameeleza vitendo vingine ni pamoja na kupigwa, kubakwa na hata kunyimwa  haki ya kumiliki au kurithi mali walizochuma na wenzi wao pindi wanapotengana katika ndoa  au mmoja wao kufariki.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment