GOLF KUTUMIKA KUJENGA MAHUSIANO. - Mazengo360

Breaking

Tuesday, 14 November 2017

GOLF KUTUMIKA KUJENGA MAHUSIANO.

SEREKALI imesema itahakikisha inatumia mchezo wa Golf kuwaunganisha watanzania na marafiki wa mataifa mengine ili kukuza ushirikiano zaidi.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kili Golf Bw. Bastiaan Bruins (Kushoto) baada ya kuwasili katika viwanja hivyo kwa  ajili ya kufunga mashindano ya Wazi ya Tanzania Kili Golf. Katikati ni  Makamu wa Rais wa Umoja wa Golf Tanzania(Tanzania Golf Union) Bw. Chris Martin.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameeleza hayo jana alipokuwa akifunga mashindano ya Kili Golf Mkoani Arusha ambapo ameeleza kuwa mchezo huo ni wa muhimu  ukazingatiwa ili ukuze zaidi mahusiano.

 “Mchezo huu wa Golf ni mzuri sana kwa kuwa unakusanya watu wa tamaduni mbalimbali na kuwaleta pamoja nami naahidi kuwa Wizara yangu itahakikisha inashirikiana kwa karibu na wadau wa Golf nchini ili kuukuza zaidi” amesema Mhe. Dkt. Mwakyembe.

Mhe. Dkt. Mwakyembe ameongoza kwa kuwataka washiriki wa mchezo huo kuwa mabalozi wazuri katika kuutangaza mchezo huo ndani na nje ya nchi na kuhamasisha vijana wengine kuwa na moyo wa kujifunza.

Mshiriki kutoka Kenya Bw. Edwin Mudanyi  akijiandaa kupiga mpira wakati wa fainali ya mashindano ya Wazi ya Tanzania Kili Golf jana Mkoani Arusha ambapo  jumla ya washiriki 250 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Afrika ya Kusini na Tanzania walishiriki.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kili Golf Arusha Bw.Bastiaan Bruins amesema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuhakikisha mchezo huo unafahamika kwa watu wengi na kuondoa dhana iliyojengeka kuwa ni mchezo wa kitajiri.

Mashindano ya Wazi ya Kili Golf Tanzania yalifunguliwa rasmi Novemba 10 mwaka huu yakiwa na jumla ya washiriki 250 kutoka nchi za Malawi, Zambia, Afrika ya Kusini, Uganda, Kenya na wenyeji akiwa Tanzania.


MWISHO.

No comments:

Post a Comment