WANA-CUF MSIRUHUSU MAWIMBI KUHATARISHA MELI YENU. - Mazengo360

Breaking

Sunday, 27 August 2017

WANA-CUF MSIRUHUSU MAWIMBI KUHATARISHA MELI YENU.

UMMA wa Tanzania mwishoni mwa juma hili umeshuhudia chama cha wananchi CUF kwa upande unaotambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini ukiruhusiwa na Mahakama Kuu kuendelea na mchakato wake wa kuapishwa kwa wabunge wake wapya nane wa viti maalum wakati wa mikutano ya Bunge inayoanza mapema mwezi ujao.

Mwenyekiti wa CUF Mhe Ibraim Haruna Lipumba pamoja na Katibu Mkuu wake Mhe Maalim Seif.
Wanahitaji lugha ya maridhiano zaidi ili kujenga tena umoja na ushiriano wa chama cha CUF, ili kiweze kustawi tena.

Kulingana na shauri lililofunguliwa mahakamani na wabunge wa CUF waliovuliwa nyadhifa zao, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa uamuzi wa kuheshimu maamuzi ya mihimili mingine, hivyo kutoa fursa kwa upande wa CUF unaoongozwa na Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kuendelea na mchakato wa kuwaapisha wabunge wapya.

Watanzania wote wenye mapenzi mema na Taifa hili, wanatamani chama hiki kikongwe cha upinzania nchini ambacho kilikuwa kikubwa wakati wa enzi zake, kirudie tena hali yake ya kupigania demokrasia nchini bila vurugu wala malumbano.

Labda tujikumbushe kidogo jinsi chama hiki kikongwe cha upinzania kilivyojikuta katika mgogoro mkubwa wa wenyewe kwa wenyewe kuanzia mara tuu baada ya uchaguzi mkuu wa Taifa wa Rais, wabunge na madiwani mwishoni mwa mwaka 2015.

Mhe Ibraim Lipumba, chama cha CUF kinakutegemea.


Mwenyekiti aliyekuwepo na ambaye hadi sasa mahakama na pia Msajili wa vyama vya siasa anamtambua kisheria, Mhe Profesa Ibrahim Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu na kujitoa katika uongozi wa chama cha CUF na baadae kutangazia umma kwamba, amestaafu masuala ya siasa na kuanza  kujishughulisha na mambo mengine ndani ya nchi na hata nje ya nchi.

Kulingana na katiba ya chama cha CUF, (ninakiri kutoipitia na kuijua inavyoeleza) wanachama wake walio upande wa CUF na wanaomtambua Mhe Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti halali, wanakiri kwamba katiba yao inaruhusu alichokifanya Mhe Ibraim Lipumba na baadae kukubalika kikatiba na kisheria kulingana na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini.

Tunawapongeza wana CUF wote pamoja na chombo chetu cha mahakama pia kwa kuweza kulishughulia jambo hili la CUF kwa umahiri na uvumilivu mkubwa na sasa tunashuhudia linafikia mwisho.

Mwishoni mwa juma hili, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Mhe Magdalena Sakaya pamoja na viongozi wengine wa ngazi ya juu wa CUF waliitisha mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salam na kuutangazia umma kwamba mgogoro huo sasa umekwisha.

Hii ni hatua nzuri na ndicho watanzania wote tunachokiombea na kukitamani.


Naibu Katibu Mkuu wa CUF Mhe Magdalena Sakaya.

Kulingana na hotuba aliyoitoa Mhe Sakaya na pia maagizo aliyoyatoa kwa umma wote, hususani kwa viongozi wa CUF ngazi zote kuanzia Taifa, wilaya, kata na vijiji alitambulisha kampeni mpya ya CUF ya kumi kwa kumi yenye lengo la kila mwana CUF kuhakikisha anatafuta wanachama wapya kumi ili kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa hapo baadae mwaka 2019 na kujipatia ushindi.

Ili kwa CUF mpya kufanikisha azma hii njema tunaomba kushauri uongozi na wanachama wote wa CUF kuchambua maneno watakayoyatumia kuwashawishi walengwa katika mpango huu.

Hii ni baada ya kusikia Naibu Katibu Mkuu wa CUF katika mkutano huo na waandishi wa habari Mhe Sakaya, bado anatumia lugha na maneno yenye ukakasi yenye kulenga kuamsha miemko na chuki baina ya wana CUF wengine na hata wasio wana CUF.

Tunapenda kuenzi na kubariki maamuzi yaliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwamba Mhe Ibrahim Lipumba kisheria ndiye Mwenyekiti halali na pia kuthibitishwa na Mhakama, hivyo tusingependa tena kutonesha yaliyopita.

Umma unatambua kwamba chama cha CUF, kabla ya kugawanyika kilikuwa kimoja na tena chenye nguvu kubwa chini ya Katibu Mkuu Mhe Maalim Seif na akishirikiana na viongozi wengine hivyo ni vizuri kunuia kusahihisha yaliyojitokeza na kujijenga upya kiwe tena kitu kimoja.

Pia, tunaelewa kwamba chama cha CUF kabla ya kuingia katika mgogoro wa wenyewe kwa wenye walikuwa na mahusiano ya pamoja na vyama vingine vya siasa hadi hata kuunda umoja uliojulikana kama UKAWA na kufanikiwa kujipambanua kutekeleza mambo kadha wa kadha kwa pamoja na waliweza, ni vizuri sasa kutibu majeraha na kuangalia kwa pamoja namna ya kusonga mbele.

Ni wazi kwamba katika mahusiano haya CUF na vyama vingine yalileta taswara nzuri ya kujenga umoja ili waweze kufikia azma ya kupata ushindi katika chaguzi mbalimbali, hili lilikuwa jambo jema kwani umoja siku zote ni nguvu na pia watanzania wote tunaombea amani na umoja udumu baina yetu bila kujali tofauti zetu za kivyama, kiimani na kijamii.

Kwa CUF mpya kuendelea kutumia lugha za ukakasi zinazoashiria utengano, vitahatarisha umoja mnaotaka kuujenga upya ili muwe kundi kubwa lenye nguvu.

Ni vizuri viongozi na wanachama wote wa CUF nchini mkiongozwa na mwenyekiti Mhe Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu Mhe Magdalena Sakaya mkajiwekea mikakati ya ndani ikiwemo michakato ya kukiimarisha chama tena ikiwamo aina na lugha itakayotumika ili kuwashawishi wengine wawakubali.

Ni wazi kwamba matendo yetu mapya ndio yatakayowashawishi mpate wanachama wengi wapya na hivyo kutimiza azama ya kampeni ya kumi kwa kumi na kujipatia ushindi mwakani kwenye chaguzi za viongozi wa mitaa na baade kuwatumia kukijenga chama tayari kwa uchaguzi mkuu ujao.

Mkiweza kufanya hivi, hata vile vyama vingine mnavyov vilalamikia kuingilia mambo na katiba yenu vitashindwa na kukaa kimya na baadae kubakiwa na aibu. Tuepuke visasi, tusikumbuke yaliyotokea, tuvumuliane na kushauriana kwa pamoja kwa lugha za staa na zenye kulenga kujenga na si kubomoa.

Nashauri pia kwamba, hata kauli mbiu yenu inayosema “CUF ngangari” mnaweza kuipitia upya na kuitathmini kama inaendana na wakati uliopo na ikibidi mje na kauli mbiu mpya inayolenga maridhiano zaidi.

Ni dhamira ya watanzania wote kuona umoja, amani na mshikamano wa Taifa unadumishwa kupitia nyanja ya siasa hususani kwa vyama kuhubiri upendo, mshikamano na umoja ambazo ndio tunu zetu za Taifa.

Tukishindwa kutekeleza haya, tukaendeleza malumbano, kukejeliana na kubezana, ni wazi kwamba watanzania mnaowalenga wajiunge nanyi amtawapata na baadae mtakapofanya tathmini hususani baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa mtajikutana hamjapiga hatua yeyote mbele.

MUNGU IBARIKI TANZANIA PAMOJA NA WATU WAKE WOTE.





No comments:

Post a Comment