TAASISI isiyo ya
kiserikali inayoundwa na Jumuiya za Wanawake wa Vyama vyote vya siasa (Ulingo)
imelaani vitendo vya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii vinavyofanywa na
baadhi ya watu dhidi ya viongozi wanawake ambao ni wanasiasa pamoja na watendaji
serikalini kwa ujumla.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na mjumbe wa Sekretarieti ya Ulingo Saum Rashid alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa aajili ya kulaani watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima viongozi wanawake.
“Matusi
ambayo wanatupiwa na watu wasio na maadili ni matusi siyo kwa wahusika tu bali
kwa wanawake wote, hivyo ikumbukwe kuwa hao wanaowalenga wanafamilia, watoto na
marafiki na wanaongoza mamilioni ya watanzania,” alifafanua Bi. Saum.
Akizungumza
bila kuwataja wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kudhalilisha viongozi,
Bi.Saum alisema wanawake wanapodhalilishwa hasa na wanawake wenzao inawakatisha
tamaa katika kutimiza majukumu yao hivyo akaomba mamlaka husika kusimamia
Sheria ili mitandao isitumike vibaya.
Aidha
Bi. Saum amesema kuwa anaamini viongozi wanawake ambao wamepewa heshima na
dhamana ya kuongoza, wana uwezo mkubwa na wanastahili kuwa kwenye nafasi walizo
nazo .
Taasisi
hiyo ambayo inawashirikisha pia watu wenye ulemavu imelaani vikali vitendo vya
udhalilishaji na kuwataka watanzania warejee kwenye misingi ya utu na
kuthaminiana kama maadili ya kitanzania yanavyoelekeza hasa kwa watoto wa kike.
Kwa upande wake mjumbe wa taasisi hiyo Angelina Mutahiwa alisema, mwanamke ndiye mlezi wa maadili katika jamii hivyo kumdhalilisha ni kuvunja malezi na maadili na kuchochea vitendo viovu dhidi yake ambavyo ameeleza vinaweza kudumu kizazi hadi kizazi.
“Wale
wachache ambao wameonesha utovu wa nidhamu kwa kuendelea kumnyanyasa mwanamke
watambue kwamba wao hawapo juu ya sheria na katiba ya nchi iko wazi hairuhusu
mwanamke kudhalilishwa, kuonewa wala kufanyiwa vitendo vya kikatili haikubaliki
na hatutakubali,” alisistiza Bi.Mutahiwa.
Ulingo
ni taasisi isiyo ya kiserikali inayoundwa na jumuiya za wanawake wa vyama vyote
vya siasa vilivyosajiliwa kwenye na Msajili wa vyama vya siasa hapa nchini kwa
lengo la kuwajengea uwezo wanawake katika nyanja mmbalimbali ili waingie kwenye
vyombo vya maamuzi.
Taasisi
hiyo kwa sasa inapigania haki sawa kwa wanawake yaani 50/50 kwani waaamini kuwa
uongozi ni haki ya kila mtu kwa maana ya wanawake na wanaume.
MWISHO
No comments:
Post a Comment