MATAMKO YATAHARIBU UPELELEZI WA LISSU. - Mazengo360

Sunday, 10 September 2017

MATAMKO YATAHARIBU UPELELEZI WA LISSU.

TAIFA lipo katika tafakari kubwa ya kujua haswa waliomshambulia kwa risasi Mhe Tundu Lissu ambaye ni Rais wa TLS na Mnajimu Mkuu wa kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki-CHADEMA.

Shaka+UVCCM+1

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka akitoa tamko  dhidi ya BAVICHA kuhusu kushambuliwa kwa Mhe Tundu Lissu leo jijini Dar.

Ni hivi juzi tuu siku tatu zilizopita akitokea kwenye vikao vya bunge mjini Dodoma, Tundu Lissu alishambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi na kumdhuru vibaya mwili wake.

Tunamshukuru Mungu kwa kuyanusuru maisha ya mbunge huyu baada ya kumiminiwa zaidi ya risasi 30 akiwa kwenye gari lake na kati ya hizo, tano zilimpata sehemu za miguuni na tumboni, kulingana na taarifa ya madaktari na polisi.
Tunaishukuru serekali kwa maana ya wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto akiwemo Waziri wake Ummy Mwalimu na Katibu Mkuu wake Dkt Mpoki Ulisyubisa pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt James Charles na madaktari wote wa hospitali ya rufaa ya Dodoma.

Pia shukrani za dhati ziende kwa viongozi kwa chama cha CHADEMA hususani mwenyekiti wake na mkuu wa kambi ya upinzani bungeni Mhe Freem Mbowe pamoja na wasaidizi wake walivyoshirikiana vyema na madaktari kusaidia kunusuru maisha ya Mhe Tundu Lissu hospitalini Dodoma.

Salamu zingine za shukrani zimwendee pia Spika wa Bunge letu Mhe Job Ndugai na wabunge wote pamoja na jeshi zima la polisi mkoani Dodoma na kote nchini kwa ushirikiano mkubwa na muhimu waliouonyesha na pia kwa msako mkubwa unaoendelea wa kuwapata waalifu waliofanya tukio hili.

Katika hali inayoashiria umma mzima kushikwa na butwaa kwa yaliyo mpata kiongozi huyu, watu wengi wamekuwa muda wote wakitamani kupokea taarifa mpya kila kuchao kuhusu maendeleo ya afya ya Mhe Tundu Lissu huko aliko hospitalini jijini Nairoi Kenya.

Hali kadhalika jamii inatarajia kwa hamasa kubwa kusikia toka kwa jeshi la polisi habari za kukamatwa kwa waalifu hao na kisha kuwafikisha katika vyombo vya sheria hapa nchini.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi mjini Dodoma hapo jana kwa waandishi wa habari zilieleza kwamba, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 25 ambapo silaha iliyotumika ni ya kijeshi aina ya SMG.

BAVICHA+TAMKO

BAVICHA wakitoa tamko lao juu ya kushambuliwa Mhe Tundu Lissu hapo juzi jijini Dar.

Hali kadhalika hapo juzi jijini Dar es Salaam, chama cha upinzani cha CHADEMA kiliitisha mkutano na waandishi wa habari na  kutoa tamko rasmi la chama kupitia Katibu Mkuu wake Dkt Vicent Mashinji juu ya tukio hilo.

CHADEMA katika mkutano huo waliliomba jeshi la polisi kuwatafuta na kuwabaini wote waliomshambulia Mhe Tundu Lissu kwani wao ndio wenye dhamana ya kisheria ya kufanya hivyo na pia walitishia kwa kusema inawajua wanaofanya vitendo hivyo.

Kupitia taarifa hiyo ya CHADEMA, ni wazi umma unazidi  kujiuliza kwa hamasa kubwa kutaka kujua ni nani au akina nani walitenda uovu huu ambapo si kawaida kwa jamii yetu ya kitanzania, ambapo imelitia doa Taifa.

Wakati huo huo CHADEMA kupitia kwa wawakilishi wake wanao muuguza Tundu Lissu jijini Nairobi wakatoa taarifa ya maendeleo ya afya ya Lissu kupitia kwa mwenyekiti wao Freeman Mbowe,ambapo ilisema aliweza kufumbua mdogo na kuongea machache.

Taarifa hizi ni wazi zinaamsha zaidi hamasa ya watu kutaka kujua zaidi ukweli uliofichika baina ya aliyeshambuliwa na waliomshambulia pia.

Pia mwishoni mwa juma hili kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar , Askofu Joseph Gwajima alitoa taarifa ya kusudio la kuendesha ibada maalum jumapili ya leo ili kumwombea Tundu Lissu jambo ambalo tayari ameshalitekeleza.

Hakuna asiye mfahamu Askofu Gwajima kwa uwezo wake wa kuhamasisha  waumini wake na hata kuteka hisia za watu wengine kumfuatilia atakalosema katika mahubiri yake.

Katika ibada yake hiyo ya leo, Askofu Gwajima amefanya pia maombi maalum ya kuwaombea kwa Mungu wale wote waliopanga kumdhuru Tundu Lissu na wasiweze kumwangamiza, na kuomba mabaya hayo yawarudie wenyewe hao waliopanga kuwaangamiza.

Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na mdogo wake wa kuzaliwa Tundu Lissu pamoja na mbunge wa Ubungo Mhe Sued Kubenea, Askofu Gwajima ameahidi pia kwenda kumtembelea rasmi Tundu Lissu hospitalini jijini Nairobi Kenya mwanzoni mwa juma lijalo ili kumfariji na kumfanyia maombi maalum ya uponyaji.

Kama tulivyosema jamii ipo katika ombwe la kupata taarifa hizo mbili muhimu, ikiwamo taarifa ya maendeleo ya afya ya Tundu Lissu na pia kusikia taarifa ya kukamatwa kwa waliotenda uovu huo.

Hapo jana jumamosi Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, SACP Gilles Muroto aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kutoa maagizo matatu muhimu.

RPC+Dodoma-+SACP+Muroto

                 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP Gilles Muroto.

Maagizo hayo ni pamoja na kutakiwa kuripoti upesi polisi kwa dereva wa Tundu Lissu aliyemtaja kwa jina moja la Adam pamoja na Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt Vicent Mashinji kufika  polisi ama mkoani Dodoma au Dar katika ofisi za upelelezi wa makosa ya jinai ili kutoa taarifa za awali zitakazoisaidia polisi kuwapata waalifu hao.

Pili, aliagiza yeyote mwenye taarifa au fununu za waliofanya tukio hilo la kumshambulia Tundu Lissu wafike polisi ili wazitoe bila kusita au kuhofia lolote, ili ziisaidie polisi katika upelelezi na tatu, jamii itoe nafasi kwa jeshi la polisi kufanya kazi yake bila kuingiliwa, alieleza Kamanda Muroto Gilles.

Maagizo haya ya polisi ni ya dhahiri na pia yapo kisheria ambapo yatasaidia sana kudumisha hali ya utulivu katika jamii nchini na pia kurahisisha upelelezi.

Hivyo basi, kufutia baadhi ya matamko mbalimbali yanayo endelea kutolewa na watu binafsi, vikundi au taasisi ambapo yanaweza kuhatarisha au kuathiri upelelezi wa polisi juu ya jambo hili, ni vizuri hatua ikachukuliwa kuyapiga marufuku.

Japo ni haki ya kila mmoja wetu kikatiba na kisheria kueleza hisia za mtu kwa wengine na hata pia haki ya kupokea na kutoa maoni binafsi, ni vizuri serekali ikalifanya hili kwa maana njema ya kutunza amani na utulivu kwa muda ili kupisha upelelezi.

Katika hili pameibuka pia makundi mawili makubwa yaliyoanza kujitokeza mitandaoni mfano facebook,twitter na intergram na wengine kufanya mikutano ya kihalisia na waandishi wa habari na kutoa matamko yenye vionjo vya mlengo wa kisiasa hususani kwa upande wa chama tawala CCM na chama cha upinzani CHADEMA.

Ukitafakari kwa kina taarifa zinazotolewa au matamko hayo, yana lenga au kuashiria kushambulia upande mwingine wa pili wa kundi la kisiasa, kitu ambacho baadae panaweza kutokea uhasama wa  makundi haya ya kisiasa.

Juzi BAVICHA kwa upande wa CHADEMA walitoa taarifa au tamko la vijana kuhusu kushambuliwa kwa Tundu Lissu ambapo pia walitoa shutuma kwa baadhi ya viongozi wa serekali na jeshi la polisi kwamba hawashughulikii ipasavyo kuwapata waliomshambulia Lissu.

Nao leo jumapili, UV-CCM  wamekuja na tamko lao wakiwashutumu BAVICHA kwa kuwashambulia viongozi wa serekali na kusema zaidi kwamba, huo ni utovu wa nidhamu kwa viongozi wa nchi.

UV-CCM walienda mbali zaidi ambapo wamempongeza kwa dhati mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kwa kuonyesha ukomavu wa kiuongozi hususani kwa rai yake aliyoitoa juzi (Mbowe) kwa umma kwamba, “katika tukio la kushambuliwa kwa Mhe Tundu Lissu pasiwepo na yeyote wa kumnyooshea mwingine kidole kwa sasa”, waliongeza UV-CCM katika tamko lao.

Katika kushutumiana makundi haya ya kivyama, baadae hakuta mwacha mtu salama.

TUNDU+LISSU
Mhe Tundu Lissu, Mnajimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki-CHADEMA ambaye pia ni Rais wa TLS.

Kwa kuzingatia baadhi ya taarifa au matamko yaliyobainishwa, ni vyema jeshi letu la polisi nchini likayapiga marufuku kwa muda, ili kuruhusu hali ya utulivu na amani iendelee kuwepo na kurahisisha upelelezi.

Aidha, Ni vizuri pia serikali kupitia jeshi la polisi, kwa vile ndilo linalofanya upelelezi huu kisheria, likae na kupanga na CHADEMA kuhusu msemaji mmoja maalum katika jambo hili kuliko kila mmoja kuibuka na kutoa tamkoa, kwa vile wao ndio wanao muuguza Mhe Tundu Lissu kwa kushirikiana na familia yake.

Hivyo taarifa kutoka kwa watu binafsi, vikundi,  taasisi au vyama vya kisiasa zizuiliwe kutolewa holela kwa muda huu hadi hapo polisi itakapokamilisha upelelezi na pia afya ya mgonjwa kuimarika kabisa.

Tumeshuhudia BAVICHA, UV-CCM, Kanisa la Ufufuo na Uzima, pamoja na ndugu yake Tundu Lissu na hata Mbunge wa Ubungo Mhe Kubenea wakitoa matamko mbalimbali au misimamo binafsi ambapo ni hatari kwa upande mwingine pamoja na utulivu wa jamii.

Hali kadhalika, ni vizuri serekali ikatoa taarifa rasmi kwa umma wa kimataifa ili kuondoa ukakasi wa taarifa zinazosambazwa na vyombo vya habari vya nje , ambapo vingine vimeeleza kwamba demokrasi nchini Tanzania imeshuka mno baada ya shambulio hili, ambapo si kweli.

Kwa kufanya hivyo, serekali itaondoa utata utakaotafsiriwa kutoka kwenye taarifa hizi potofu hususani kwa nchi marafiki,wafadhilina hata mabalozi wa nje.

 “MUNGU ENDELEA KUTULINDA NA KUTUEPUSHA NA MABAYA.”

                                                    (Picha kwa hisani ya Ayo Tv).