SIMAMA KATIKA JARIBU LAKO. - Mazengo360

Breaking

Monday, 13 November 2017

SIMAMA KATIKA JARIBU LAKO.



KILA mwanadamu kuna wakati hupitia katika majaribu ya aina mbalimbali katika maisha yake. 

Nguvu katika Majaribu.
Kuna majaribu ambayo huja kwa sababu kuu zifuatazo:
1. Kupunguza kufanya maombi pamoja na ibada,
2. Kuna majaribu yanayotokana na hila za watu,
3. Kuna majaribu yanayotokana na tamaa ya mtu mwenyewe,
4. Kuna majaribu kama kipimo cha MUNGU kwa mtu wake ampendae.
Je? Jaribu unalopitia kwa sasa lina sababishwa na ipi hapo juu?
Je? Kwa nini tunashindwa kupata ushindi katika majaribu?

Zifuatazo ni sababu kuu 5 za mtu kushindwa katika majaribu na hapa tunajifunza kwa kupitia  mtumishi wa MUNGU Ayubu.

1: WAHUDUMU WETU KATIKA MAJARIBU.

Ayubu 2:9.

''Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe''

 Hapa mke wa Ayubu ambaye alitakiwa awe ndiye anayemtia moyo mmewe, yeye ndiye anamshauri amkufuru MUNGU ili afe.
Na hata leo wapo watu wengi sana ambao yawezekana uko kwenye jaribu fulani mfano ugonjwa lakini wao ndio wanashauri kwamba uende kwa mganga wa kienyeji ukazindikwe ili upate nafuu, kumbe ndio kabisa wanakupoteza.
Hivyo  wahudumu wanaweza kabisa wakasababisha ushindwe katika jaribu fulani hata kama ni dogo.
2: MARAFIKI ZETU WAKATI WA MAJARIBU.

Ayubu 2:12-13''

Basi walipovua macho yao, nao wakali mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho yake, wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni. Kisha wakaketi nchi pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye neno lo lote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.''

 Marafiki wakati mwingine wanaweza kuwa kikwazo cha mtu kushinda jaribu alilonalo na hapa tunajifunza kuhusu marafiki watatu wa Ayubu ambao walikuja kumtembelea.
Badala ya wao kuwa faraja ndio kwanza walianza kumshutumu Ayubu kwamba haiwezekani awe hivyo lazima tu kuna dhambi amefanya na wanamwambia awaambie dhambi aliyofanya ili wamwombee kwa MUNGU ili jaribu lake liishe, kumbe wao ndio wakosaji na sio Ayubu.
Ndugu, ni mara ngapi umepatwa na magumu na marafiki zako kuanza kukushutumu kwamba haiwezekani MUNGU ayaruhusu hayo kwako?
Wao hujiona wapo wakamilifu mno na tena kusema, “ ni lazima tu umetenda kosa na Mungu akakuadhibu, kumbe hata hukutenda lolote ila ni jaribu tu la kupima imani yako.
Hivyo, marafiki au watu wanaokutembelea wakati wa jaribu wanaweza kuwa sababu yako ya kushindwa kama ukiamua kuwasikiliza wakuambiacho.
Hapa Ayubu hakuwapa nafasi; ndio maana alishinda majaribu hayo.

Unaweza ukajiuliza kati ya Ayubu na wale rafiki zake ni nani alikua  na mashaka? Ayubu alikua jasiri bila mashaka yeyote katika imani.
Marafiki zake walikua na mashaka kuliko hata mgonjwa mwenyewe na kama uko kwenye hali mbaya halafu wazima waliokuzunguka wao ndio wanalia hata wanashindwa kula, hakika watazidisha ugonjwa kwako ukiwasikiliza.
3: KUJIHESABIA HAKI WAKATI WA MAJARIBU.

Ayubu 9:2

''Kweli najua kuwa ndivyo hivyo; Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?''

Usijihesabie haki wakati wa jaribu na pia ndugu walio chini kiroho  usiwasikilize sana wakati huo maana imani zao ni ndogo hivyo ni rahisi sana kukukatisha tamaa na kukufanya uchukue maamuzi mabaya, tena ukiwa karibu kabisa na ushindi wako.

4: TUSIJILINGANISHE NA WASIO PITIA MAJARIBU.

Ayubu 12:4

''Mimi ni mtu wa kuchekwa na jirani yake, Ni mtu niliyemwita Mungu, naye akanijibu; Huyo mwenye haki, aliye mtimilifu, amekuwa ni kicheko''

 Ndugu, usikubali  kujilinganisha na watu ambao hawajaribiwi wakati huo maana unaweza ukaanza kulalamika na kusababisha  ukufuru kwa MUNGU, na kujiona kama unaonewa wewe tu huku wengine wakiishi kwa amani na furaha isipokua wewe tu.
Elewa Mungu hapendi manung’uniko bali shukrani zaidi na pia kumtumainia yeye bila mashaka yawae yote.
5: TUSIWAHUSUDU WASIOAMINI.

Ukiwahusudu wasio amini utakuwa unajipoteza wewe mwenyewe kuufikia ushindi wako, pia ukiwahusudu wasio amini utakua unaanza kuikataa ukweli au mbingu na kujitoa katika IMANI.

“SIMAMA KATIKA JARIBU LAKO KWA IMANI, UTASHINDA”

(Kwa hisani ya mtanado na mchambuzi Peter Michael Mabula).

No comments:

Post a Comment