MAASKOFU KATOLIKI WATOA TAMKO. - Mazengo360

Breaking

Monday, 11 September 2017

MAASKOFU KATOLIKI WATOA TAMKO.

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa taarifa yake ya tamko la kulaani vikali vitendo vya kikatili vinavyoendelea kutokea  hapa nchini hivi sasa na  kuitaka serekali kukomesha mara moja vitendo hivyo.

Maaskofu Katoliki Nchini wakiwa katika moja ya shughuli zake za uinjilishaji.

Katika taarifa ya maandishi iliyotolewa mchana huu na kutumwa kwenye vyombo vya habari na kusainiwa na Makumu Rais wa TEC, Askofu Mkuu Beatus Kinyaia wa Jimbo la Dodoma iliyataja matendo hayo ikiwamo lile la kushambuliwa kwa mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.


Matendo mengine yaliyotajwa katika taarifa hiyo ambapo ni maamuzi ya mkutano wa kawaida wa maaskofu hao uliofanyika makao makuu ya TEC Kurasini jijini Dar mwezi huu tarehe 8-9 ni pamoja na mauaji ya watu huko Mkuranga, Rufiji na Kibiti.

Mengine ni utekwaji wa watu na kuteswa, utekaji wa watoto wadogo na kuwaua baadhi yao pamoja na ulipuaji wa ofisi za watu, taarifa hiyo ilifafanua zaidi.

Maaskofu hao wamesema, “tunapenda kutamka wazi na kwa nguvu zetu  zote kuwa vurugu na mashambulizi ya aina yeyote ile yanalifedhehesha Taifa” taarifa hiyo ilisisitiza.

Hapa nchini hususani kwa mwaka huu kwa vipindi vinavyokaribiana sana, matendo ya kikatili yasiyo ya kawaida kwa utamaduni wa watanzania yamekuwa yakishamiri mno na kusababisha hofu kubwa katika jamii.

Hali kadhalika kwa hivi sasa, jamii inaendelea kutafakari kitendo cha kushambuliwa kwa risasi kwa Mnajimu Mkuu wa kambi ya Upinzani bungeni na Rais wa chama cha wanasheria nchini (TLS) Tundu Lissu.

Shambulizi hilo lilitoke katikati ya makao makuu ya serekali mjini Dodoma majira ya saa saba unusu mchana akitokea kwenye vikao vya bungeni alipokuwa akiingia nyumbani kwake Area D.

Taarifa hiyo imetoa pole nyingi kwa wahanga wote na pia kuwatakia kupona haraka kwa wale waliojeruhiwa, na kuahidi kuendelea kuwaombea zaidi, ilimalizia taarifa hiyo.


MWISHO.

No comments:

Post a Comment