PROFESA Joyce
Ndalichako, Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia ameitaka Mamlaka ya Elimu, na
Mafunzo ya Ufundi Stadi -VETA -kurejesha haraka fedha ambazo ni masurufu
kiasi cha shilingi Milioni 600 ambazo hazionekani kwenye kumbukumbu na wala
hazina maelezo kuwa zimetumikaje.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo mkoani Dodoma wakati akizungumza na menejimenti ya Taasisi hiyo mkoani Dodoma ambapo amewataka wale wote waliohusika na kutumia fedha hizo wazirejeshe na ziweze kufanya kazi iliyokusidiwa vinginevyo fedha hizo zikatwe kwenye mishahara yao.
Waziri Ndalichako amesema
haridhishwi na uwajibikaji wa Taasisi hiyo kutokana na kushindwa
kusimamia shughuli za utekelezaji na badala kufanya kazi kwa mazoea.
Waziri Ndalichako ameitaka VETA
kuhakikisha inafanya uhakiki wa vyeti kwa kuwa hayo ni maagizo ya
Serikali kwa nchi nzima, pia ameelekeza kama zipo taasisi zilizochini ya
Wizara yake na hazijafanya uhakiki zifanye haraka.
Wajumbe wa mkutano huo wa uongozi wa VETA wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Prof Joyce Ndalichako alipokuwa akiwahutubia leo mjini Dodoma. |
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo Peter Maduki amezungumzia suala la uwajibikaji na utendaji kazi ambapo menejimenti imekubaliana kuwa dhana ya ugatuwaji iimarishwe ambapo wamekubaliana kuwa watasambaza waraka ili watumishi wa Taasisi hiyo wausome na kutoa maoni kwa lengo la kuboresha hadi ifikapo Novemba 30, 2017.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment