WAZIRI wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewapongeza
Wajasiriamali wa Tanzania kwa ushiriki wao katika Tamasha la Utamaduni na Sanaa
Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST linalofanyika jijini Kampala Uganda.
Dkt. Mwakyembe ametoa
pongezi hizo jana katika viwanja vya Mashujaa Kololo jijini Kampala alipotembelea
kujionea namna tamasha hilo lilivyopokelewa na wadau wake walioiwakilisha
Tanzania wakiwemo wajasiriamali toka vikundi mbalimbali, vikundi vya ngoma,
vikundi vya sanaa ya maigizo pamoja na baadhi ya wasanii.
Katika tamasha hilo, Dkt.
Mwakyembe pia alipata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya wajasiriamali
hao pamoja na kuongea nao huku akijionea bidhaa mbalimbali zinazouzwa na nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jambo ambalo limemfurahisha sana
hususani kwa upande wa watu kutoka Tanzania kwakuwa wamejaza mabanda yao kwa
bidhaa kadha wa kadha.
“Tamasha hili linaonyesha
utajiri mkubwa wa sanaa, utamaduni pamoja na bidhaa tulizonazo kama nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na hapa tumekutana kwasababu
tunabadilishana mawazo na kuonyeshana bidhaa mbalimbali za nchi zetu”, alisema
Dkt. Mwakyembe.
Aidha, katika ziara hiyo,
Dkt. Mwakyembe amewatoa wasiwasi wajasiriamali hao kuhusu suala la upatikanaji
wa masoko huku akiwaahidi kuwatafutia fursa ya kuwapeleka wajasiriamali hao
pamoja na bidhaa zao Bungeni mjini Dodoma ili ziweze kupata soko kwa urahisi
kupitia wabunge.
“Niwatoe wasiwasi
wajasiriamali wote wa Tanzania mliohudhuria hapa, nitahakikisha kuwa pindi
tunaporudi nyumbani nitatafuta wasaa wa kulishawishi Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ili nyie mpate nafasi ya kuleta bidhaa zenu katika viwanja
vya Bunge ili basi Wabunge wapate kujua haswa vitu vizuri mlivyonavyo nah ii
itawasaidia kuviuza kwa urahisi zaidi na kujipatia vipato vyenu”, aliongeza
Dkt. Mwakyembe.
Sambamba na hilo, Dkt,
Mwakyembe amewahakikishia wajasiriamali hao kuhusu suala la kujitangaza kupitia
vyombo vya habari akisema kwamba, atajitahidi kutoa ushawishi kwa vyombo vya
habari nchini ili viweze kuwapatia muda wa kuwatangaza wajasiriamali hao ili
wapate kujulikana ikiwemo shughuli wazifanyazo.
“Nitahakikisha kuwa siku
mnapopewa nafasi ya kuja viwanja vya Bunge basi mnapata muda wa kutosha katika
vyombo vya habari ili mpate kujulikana, hivyo kila mmoja wenu naamini atapewa
nafasi ya kufanya mahojiano kwa kujieleza shughuli azifanyazo na mahali
anapopatikana na hii itawasaidia kupata masoko zaidi toka kwa watu mbalimbali”,
alisema Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wao
wajasiriamali hao wameshukuru Waziri Mwakyembe kwa juhudi alizowafanyia
hususani za kuhakikisha kwamba wanahudhuria kwa kiwango kikubwa katika tamasha
hilo, lakini pia ahadi aliyowapa ya kuwapeleka Bungeni ili wakatangaze bidhaa
zao na kuwatangaza katika vyombo vya habari nchini.
Tamasha la JAMAFEST
lilianzishwa mwaka 2013 nchini Rwanda na baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki ambapo kwa mwaka huu tamasha hilo linafanyika mjini Kampala
nchini Uganda ambapo pia tamasha hili linatarajiwa kufanyika tena katika moja
ya nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2019.
(Habari hizi na picha kwa hisani ya Idara ya Habari Maelezo).
MWISHO
No comments:
Post a Comment