SERIKALI kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo ya watoto wa kike hapa nchini wameendesha
mafunzo kwa waendesha bodaboda walioko wilaya ya Tarime mkoani Mara
kuwahamasisha vijana hao kuunga mkono juhudi za kitaifa za kutokomeza
mimba za utotoni kwa wasichana walioko shule ya msingi na sekondari.
Bodaboda wakitega abiria wakiwamo wanafunzi. |
Akieleza malengo ya mafunzo hayo, Afisa Mkuu wa Maendeleo ya Jamii Bibi Anna Shengweli amebainisha kuwa madreva wa bodaboda ni kundi mahususi katika ulinzi wa watoto wa kike kwani kutokana na shughuli zao wanakutana mara nyingi na watoto wa kike wakiwa katika mazingira hatarishi.
“Wakiwa
katika kazi zao za kila siku bodaboda na wanapishana na watoto wa kike
wakitekeleza majukumu yao mbalimbali ikiwemo kwenda na kurudi kutoka shule,
kuteka maji visimani, kuchunga mifugo porini, sokoni, stendi ya basi na
kadhalika’’ alisema Bibi Anna.
Kwa
upande wake mwezeshaji kutoka ‘Shirika la Save the Childern’ Bw. John
Komba amesema kuwa ni muhimu kuwajengea uelewa waendesha bodaboda ili
wawe tayari kutambua na kutekeleza wajibu wa kuwaelimisha na kuwalinda watoto
wa kike waepukane na vitendo vya ngono wawapo nyumbani, shuleni, njiani,
sokoni, mitaani, na katika shughuli za kijamii kwa ujumla.
“Mafunzo
haya yatawasidia waendesha bodaboda kuwa mabalozi wa usalama na ulinzi wa mtoto
wa kike ili kupunguza idadi ya wasichana wanaoacha shule kutokana na changamoto
ya mimba za utotoni na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao, pamoja na
kuwashirikisha katika mtandao wa usalama wa mtoto katika ngazi ya kata na
mitaa. Juhudi hizi zikifanyika zitachangia kupunguza tatizo la mimba za utotoni
kutoka asilimia 27 hadi asilimia 8 ifikapo mwaka 2022 alisema Bw. Komba.
Naye
Mkurugenzi Mkazi Shirika la REPPSI Bibi. Edwick Mapalala amefafanua kuwa
mafunzo haya yatasaidia kumwezesha mtoto wa kike aweze kuwa na maisha bora
yenye usalama maana atahakikishiwa ulinzi na ndugu wa karibu katika familia,
watoa huduma wanaomzunguka mtoto, na jamii yote kwa ujumla.
“Mafunzo
haya yataimarisha uaminifu wa madreva wa bodaboda kuzingatia umuhimu wa kuzuia
na kupunguza matukio ya mimba za utotoni kwa watoto wa kike” alisema Bibi
Edwick.
Aidha
Mwenyekiti wa madreva bodaboda wilayani Tarime Bw. Paschal Joseph, ameishukuru
Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo pamoja na wadau mbalimbali na ameahidi
kuwaheshimu, kuwalinda na kuwapa haki sawa watoto wa kike katika ngazi ya
familia na jamii kwa ujumla.
Semina
hiyo ya siku moja iliyoandaliwa na mashirika
yautetezi haki za watoto
nchini wakiwemo UNICEF, Save the Children, Plan International Tanzania,
REPSSI na CDF na jumla ya washiriki 40 wamehudhuria mafunzo hayo kati ya vijana
1600 wanaojihusisha na uendeshaji wa Bodaboda wilayani Tarime.
Mafunzo
hayo yamefanyika ikiwa ni moja kati ya shughuli muhimu za maadhimisho ya Siku
ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike 2017 yenye kauli mbiu inayosema “Tukomeza
Mimba za Utotoni Tufikie Uchumi wa Viwanda’.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment