SERIKALI YAWASHAURI WADAU WA HABARI NCHINI. - Mazengo360

Thursday, 29 June 2017

SERIKALI YAWASHAURI WADAU WA HABARI NCHINI.

SERIKALI imewashauri wadau wote wa mambo ya habari hapa nchini kujenga umoja ili kuisaidia utekelezaji wa sheria mpya ya huduma za habari ya mwaka 2016 iweze kutumika.

Akiongea na wadau wa habari mjini Dodoma katika warsha ya siku moja iliyowashirikisha serikali na wadau wa habari nchini, Naibu Waziri wa Habri, Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mhe Annastazia Wambura aliwaeleza washiriki katika warsha hiyo umuhimu wa kuwa kitu kimoja.

Naibu Waziri alisema, “ili kuisaidia serikali kufanyia kazi baadhi ya mambo yanayoonekana kuleta ukakasi katika sheria ya huduma ya habari ya mwaka 2016, ni vizuri wadau wote tukawa na umoja, ili kusaidia ufanisi wa sheria hii,alieleza Naibu Waziri.

MISA+3

Naibu Waziri wa Habri,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe Annastazia Wambura akiwahutubia wadau wa Habari (hawapo pichani) katika warsha ya MISA mjini Dodoma jana.

Alieleza pia kwamba, serikali inayo nia njema ya kupitisha  sheria hii, ili kuboresha sekta ya habari hivyo wadau wasiione serikali kama adui kwao,bali ni kulenga kusaidia mfumomzuri wa kusimamia mambo ya habari hapa nchini kulingana na wakati uliopo,alifafanua Naibu Waziri.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Mhe Wambura aliwataka wadu wa habari kujikita zaidi katika kuzingatia maadili na miiko ya uandishi wa habari na kamwe  wasitumie kalamu zao kupotosha umma bali wazingatie ukweli.
Naibu Waziri alitolea maelezo kwa kurejea mchango wa maoni uliotolewa katika warsha hiyo na Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, Mhe  Moshi Seleman Kakoso kwamba, wadau wa habari wanakiuka maadili ya uandishi kwa kutokuwa wakweli kwa kubinya kimaudhui kwa taarifa wanazo toa.

Katika marejeo hayo Naibu Waziri alieleza wito wa Mhe Kakoso kwamba, “kuna tatizo la ukiukaji mkubwa wa kimaadili kwa baadhi ya waandishi na vyombo vya habari kwa kuweka kichwa cha habari kikubwa juu ya kurasa wa mbele wa gazeti, lakini ukienda kwa undani katika habari hiyo, hupati maelezo husika kwa kina hivyo kubinya maudhui ya taarifa hiyo na kuacha maswali mengi kwa msomaji.
Naibu Waziri alitoa wito kwamba ni vizuri wadau kuzingatia maadili ya kiuandishi ili kuzuia makali ya sheria hii mpya isije kuwagusa na  kuilamu serikali kwamba haina malengo mazuri na vyombo vya habari.

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo, Bi Zamaradi Kawawa aliwaeleza washiriki wa warsha hiyo kwamba, wadau wa habari wakiwamo wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na waandishi waipe muda sheria mpya ya huduma ya habari ya mwaka 2016 ianze kutumika kwanza, kuliko kuanza kuilalamikia ingali bado mapema.

MISA+2

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo Bi Zamaradi Kawawa akiwahutubia wadau wa Habari katika warsha ya MISA mjini Dodoma jana. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Habri Mhe Annastazia Wambura na wadu wengine.

Kaimu Mkurugenzi huyo alieleza pia kwamba, ikiwa itabainika upo ugumu wa baadhi ya maeneo katika sheria hiyo basi Idara pamoja na wadau wa Habari watakaa pamoja ili kutoa mapendekezo kwa vyombo husika vya serikali ili kuipitia na kurekebisha.

Warsha hiyo ya siku moja iliandaliwa na Wizara ya Habari kushirikiana na MISA ili kujadili njia nzuri zaidi ya kujenga mahusiano ya kiutendaji baina ya serikali na vyombo vya habari hapa nchini.

MISA+1      
  Naibu Waziri Mhe Annastazia Wambura katika picha ya pamoja na wadau wa Habari mjini Dodoma jana.

Washiriki katika warsha hiyo walikuwa wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri, waandishi, viongozi wa MISA, TMF pamoja maafisa habari wa baadhi ya Idara za serikali, wabunge na wanasheria.


MWISHO.