PINDA AMSHANGAZA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE - Mazengo360

Wednesday, 28 June 2017

PINDA AMSHANGAZA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE


IMG_20170625_122032_1CS

SERIKALI imeguswa na mfano mzuri unaoonyeshwa na ukulima wa kisasa wa Waziri Mkuu mstafaafu Mhe Mizengo Kayanza Peter Pinda na kuagiza viongozi wote kuiga na kuhimiza viongozi wa kada tofauti kwenda Zuzu Dodoma kujifunza mfano huo.

Akitoa nasaha za salamu za mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu uliokimbizwa katika Manispaa ya Dodoma nakutembelea shamba la mfano la Mhe Mizengo Peter Pinda lililopo kijiji cha Zuzu (Zinja) na kutunuku cheti cha heshima, kiongozi wa mbio hizo mwaka huu Amour Hamad Amour alieleza shamba la Mhe Pinda ni mfano wa kuigwa na viongozi wote.

Mwenge wa Uhuru uliopokelewa majira ya asubuhi hapo jana kutokea wilayani Chemba mkoani hapa Dodoma na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Christina Mndeme mbali na kutembelea shamba lamfano la Mhe Mizengo Pinda ulitembelea pia miradi kadhaa na kuizindua.
IMG_20170625_122002_1CS

Miradi hiyo ikiwamo uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko ya Kizota iliyopo mjini Dodoma pamoja na kufungua wadi ya hospitali ya kinamama iliyopo kijiji cha Makondeko na pia ufunguzi wa upanuzi wa kiwanda cha mvinyo cha Dodoma kinachotegemewa kuzalisha ajira zaidi.

Wakati huo huo, Kiongozi huyo wa mbio za mwenge alishangaa kuona uwekezaji mkubwa tena wa kisasa unaofanywa na kiongozi huyo mstaafu, Mhe Mizengo Pinda katika kijiji cha Zuzu (Zinja) ambacho pia kilibadilishwa jina kuanzia jana na kuitwa kijiji cha Zinja badala ya Zuzu na kusema, Mhe Pinda anatekeleza kwa vitendo azma ya serikali ya awamu ya tano na kusema viongozi wote hawana budi kwenda kujifunza kwa Mhe Pinda, na kueleza zaidi kwamba,

“Mhe Mizengo Peter Pinda na familia yake, si tuu wanatekeleza mfano wa ukulima wa kisasa bali ni kutekeleza fikra za Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa vitendo, ambapo ni fursa pekee kwa watanzania hususani viongozi, na hivyo waige kutoke kwake”, alieleza kiongozi huyo wa mbio za mwenge.

Aliendelea kueleza kwamba, shamba la Mhe Mizengo Pinda ni la kipekee na tena ni zaidi ya mfano kwa vile limejumuisha zaidi ya uzalishaji wa aina moja bali aina mbili au zaidi katika sekta tofauti, kitu ambacho si rahisi kuupata mahali pengine.

Alifafanua kwamba mfano huu unapatikana tuu maeneo ya mafunzo mfano mfano Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine na kueleza kwamba ataenda nyumbani alikozaliwa visiwani Zanzibar na kuwashauri viongozi wa serikali ya Zanzibar waje kujifunza kutoka kwa Mhe Mzengo Peter Pinda.

Aliwataka pia watu wote wa Dodoma kuungana pamoja na kutumia fursa hii nzuri kujifunza kwani ni nafasi hadimu itayoweza kuwasaidia kutokana na kilimo au ufugaji usio wa kisasa ambapo hakijawasaidia kutoka katika lindi la umaskini, alisema.

Nae mke wa Mhe Mizengo Peter Pinda, Mama Tunu Pinda alimweleza kiongozi huyo wa mbio za mwenge kwamba wamefarijika kupokea heshima hiyo kubwa ya kuuleta msafara wa mbio za mwenge kijijini hapo na kutembelea shughuli wanazofanya na kusema kwamba, ni kwa sababu jambo wanalolifanya ni la mfano na la manufaa kwa jamii yote.

Mama Tunu Pinda alifafanua zaidi kwamba, mafanikio waliyoyafikia hadi sasa yalianza muda mrefu tangu mwaka 2001 ambapo yeye na mmewe Mhe Pinda walianza kupangilia maisha yao baada ya kustaafu utumishi wa umma ambpo walitembelea maeneo mbalimbali hapa Dodoma mfano Makotopora, Msalato hadi Zuzu (sasa Zinja) ambapo ndipo walipo hivi sasa.

Mama Pinda alitoa wito kwa viongozi wote wa serikali kuishi kwa kuonyesha mfano wa kile wanachokihubiri kwa vitendo kwa wananchi kwa vile utakuwa mfano bora utakaowafanya waendelee kuheshimika katika jamii na kuwa na amani na watu wote na pia kuishi vizuri wakati wa kustaafu kwao.

Aidha, Mama Pinda alieleza pia kwamba kwa sasa shamba lao lina uwezo wa kutoa ajira kwa baadhi ya wanajamii wanaozunguka eneo hilo na pia kuwasaidia baadhi ya watoto walemavu pamoja na maskini wengine wasioweza kupata elimu na kuonyesha mfano halisi ya kijana anaeishi na ulemavu wa ngozi waliokabidhiwa siku nyingi na Mhe Rais John Pombe Magufuli kutokea wilaya ya Chato siku nyingi wakati Rais akiwa bado waziri, na kueleza pia kwamba huo ndio mfano wa kiongozi anavyotakiwa kuishi.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Bi Christina Mndeme alimwagia sifa mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Mama Tunu Pinda na kueleza kwamba ni mfano mzuri sana wa mwanamke anavyopaswa kufanya katika jamii na kutoa wito kwa akina mama wote nchini kuiga mfano mzuri na ujasiri wa mama Tunu Pinda.

Huku akinukuu maneno kutoka kwenye kitabu cha maandiko ya Bibilia yasemayo, “mwanamke mpumbavu huibomoa nyumba kwa mikono yake mwenyewe”, Mhe Mndeme alisema Mama Pinda ni mwerevu, jasiri na tofauti kabisa na yaliyoelezwa katika maandiko na akampongeza Mama Tunu Pinda na kuwataka akina mama wote kuiga mfano wake.

Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa katika maeneo mbalimbali ya manispaa ya Dodoma baada ya kupokelewa kutoka wilaya ya Chemba na kukesha ukiwawa katika viwanja vya shule ya msingi Ipagala,iliyopo manispaa ya Dodoma na baadae ulitegemewa kukabidhiwa wilayani Bahi kuendelea na mbio zake.

MWISHO.