KANISA KATOLIKI HALITACHOKA KUWATUMIKIA WATU. - Mazengo360

Breaking

Thursday, 2 November 2017

KANISA KATOLIKI HALITACHOKA KUWATUMIKIA WATU.

KANISA KATOLIKI limesema halitachoka kuwatumikia watu wote na wa imani zote ili kujiletea maendeleo ya kweli ya kiroho na kimwili huku likisisitiza kuishi kwa amani, umoja, mshikamano na upendo kwa watu wote ambapo ndizo tunu za taifa katika kuiletea jamii maendeleo.


Padre Chesco Msaga ambaye ni Naibu Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma (Vicar General, katikati mwenye mavazi ya kikasisi) akiwa na Naibu Waziri katika ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Vijana, Kazi na Ajira na pia Mbunge wa Dodoma Mjini Mhe Antony Mavunde (mwenye suti nyeusi) katika picha ya pamoja na viongozi wa dini zingine katika sherehe iliyoandaliwa na Parokia Katoliki ya Makole hivi majuzi mjini Dodoma. Wengine wa kwanza kutoka kulia ni Paroko Msaidizi wa kanisa hilo Padre Joseph Gele akifuatiwa na Shekhe wa Msikiti wa Makole na Mjumbe wa Baraza la Kiislamu la Wilaya ya Dodoma Mjini, Sheikh Hassan Athman Ngao (mwenye kofia na skafu) akifuatiwa na Kasisi wa Kanisa la Anglikani la Mtakatifu Bartholomayo la Makole la hapa Dodoma, Kasisi Bezalel Mbijima (mwenye stola au scaf nyekundu). Aliye karibu kabisa kulia kwa Naibu Waziri ni Ustadhi Athman Omar ambaye ni mwanafunzi wa dini ya Kiislamu toka Msikiti wa Makole (mwenye kofia na koti) pamoja na wageni wengine waalikwa hivi juzi katika sherehe hiyo mjini Dodoma.

Naibu Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma (Vicar General) Padre Chesco Msaga aliyasema hayo mwishoni mwa juma lililopita katika mahubiri yake aliyotoa wakati wa misa ya kumbukumbu ya somo wa jina la parokia ya Kanisa Katoliki la Makole lililopo mjini Dodoma ambayo hujulikana kwa jina la Parokia ya Mt Gaspar Del Bufalo, Makole Dodoma.

Parokia hiyo ipo chini ya Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma ikisimamiwa na kuendeshwa na mapadre wa Shirika lijulikanalo kama “Wamissionari wa  Damu Takatifu ya Bwana Yesu” kulingana na taratibu za Kanisa Katoliki yaani (Community of Precious Blood Fathers) ambaye mwanzilishi wake ni Mtakatifu Gaspar Del Buffalo.

Padre Chesco ambaye pia ni Vicar General wa Jimbo hilo alisema “Kanisa Katoliki kote duniani ikiwamo hapa nchini limekuwa likitekeleza mpango mkakati wake muhimu (strategic plan) wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika umaskini wa kiroho na kimwili ambapo ndio mpango wa Bwana Yesu hapa duniani” na kufafanua kwamba hushirikisha jamii ya watu wote bila ubaguzi wa imani au rangi ndio msingi haswa, alisema.


Mgeni mwalikwa toka moja ya dini zingine Shekhe wa Msikiti wa Makole na Mjumbe wa Baraza la Kiislamu la Wilaya ya Dodoma Mjini, Sheikh Hassan Athman Ngao (mwenye kofia na skafu) akisalimiana na Padre msaidizi wa Parokia ya Kanisa Katoliki  la Makole Padre Antipas Shayo (amekingwa na Kasisi wa Kianglikana) wakati wa wageni kupeana salamu katika sherehe iliyoandaliwa na Kanisa hilo hivi majuzi mjini Dodoma. Anayeshuhudia katikati ni Naibu Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma ambaye kikanisa ni Vicar General Padre Chesco Msaga akitabasamu pamoja na wageni wengine.

Aliongeza kwa kutoa pia mfano jinsi walivyowashirikisha waalikwa mbalilmbali kutoka katika dini na imani zingine kufurahi nao katika maadhimisho hayo siku hiyo ambapo Padri Chesco alifafanua kwamba ndiyo malengo ya kanisa kwa watu wote kukaa pamoja kwa amani na kufurahia upendo huku  jamii ikijitahidi kupata uelewa mpya wa kutoka katika umasikini na kufikia maendeleo.

Pia alisema, binadamu hawezi kukombolewa bila kupewa elimu itakayo mwezesha kupata uelewa wa kutosha kupambanua mambo katika jamii ili maisha yawe rahisi na kuongeza kwamba ndio maana kanisa hujenga mashule,mahospirtali, vituo vya mfano vya mashamba na uzalishaji mali kupitia miradi mbali mbali, huo ndio mkakati wa kanisa kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili alisema Padre Chesco Msaga.

“Kila mmoja wetu ni shuhuda katika jambo hili ambapo shule na hospitali pamoja na maendeleo mengine ya jamii yamekuwa yakitekelezwa na kanisa Katoliki Katika jamii kwa kusaidiana na Serekali pamoja na wadau wengine wa maendeleo, na kuongeza kwamba huko ndiko kumkomboa mwanadamu” alifafanua Padre Chesco.


Baadhi ya sehemu ya waimbaji wa Kwaya Shirikishi ya Kanisa Katoliki Parokia ya Makole ya Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma wakiimba kwa furaha  katika adhimisho la ibada ya Misa iliyowashirikisha wageni toka sehemu mbalimbali na imani tofauti hivi karibuni parokiani hapo mjini Dodoma.


Hivyo ametoa ushauri kwa jamii nzima ya watanzania kuendelea kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha lengo la kanisa pamoja na la serekali la kuwaletea watu maendeleo hayo linafikiwa kwa kushirikiana na jamii yote bila kubaguana, aliongeza Padre Chesco.

Akitoa salamu za serekali katika sherehe hizo Naibu Waziri katika ofisi ya Waziri Mkuu; Vijana, Kazi na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini (CCM) Mhe Antony Mavunde amelipongeza kanisa kwa jinsi linavyoshirikiana na serekali kuwaletea wananchi wake maendeleo.

“Serekali inalipongeza kanisa kwa kutekeleza vyema suala la jamii kuishi kwa amani, umoja na mshikamo kama waasisi wa Taifa letu walivyohimiza tangu nchi ipate uhuru wake na kuomba waendelee kufanya hivyo” alieleza Mhe Mavunde.

Alisema pia kwamba serekali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na madhehebu ya dini ikiwamo Kanisa Katoliki katika utoaji malezi na elimu kwa jamii ili kuwaletea maendeleo.


Baadhi ya watu waliohudhuria sherehe hizo wakiwamo akina mama, watoto, vijana na hata walinda usalama wakiwamo “Polisi wa Trafiki” katika sherehe ya kukumbuka somo wa Parokia ya Mtakatifu Gaspar Del Bufalo ya Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma iliyofanyika hapo parokiani Makole hivi majuzi mjini Dodoma.

Pia amepongeza jinsi kanisa linavyoishi na jamii za imani nyingine kwa upendo na kushirikiana katika yote bila ubaguzi na kuongeza kwamba huo ni mfumo mzuri unaofaa kuigwa, alisema Mhe Mavunde.

Wamisionari wa Shirika la Mapadre wa  Damu Aziz ya Bwana Yesu (Missionaries of Precious Blood Fathers) ambao wanafanya huduma zao maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwamo Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, walifika mkoani Dodoma mara ya kwanza mwaka 1967 ambapo mwaka huu wanatimiza nusu karne.

Mapadre wa shirika hilo ndio pia waliojenga kanisa kuu la Jimbo la Dodoma la Mtakatifu Paulo wa Msalaba na pia wanaendesha miradi mingi ya kijamii ikiwamo mashule, hospitali, kituo cha Radio yaani Mwangaza Radio FM pamoja na hoteli na kumbi za mikutano cha St Gaspar Hotel cha mjini Dodoma.


MWISHO. 

No comments:

Post a Comment