WATUMISHI wa
Idara zilizopo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
wametakiwa kufanya kazi zao kwa bidii na weledi mkubwa katika kutekeleza wajibu
wao kwa umma na wametakiwa kamwe wasikiuke maadili ya utumishi wa Umma.
PS Suzan Mlawi, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. |
Nasaha hizo zimetolewa leo
mjini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi.Suzan Mlawi katika kikao na
watumishi wa Wizara ambapo amewahamasisha kufanya kazi kwa bidii ili kufikia
malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananchi kupitia sekta zilizo chini ya
wizara hiyo.
“Endeleeni kuwa waadilifu
na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, ni wajibu wa kila mmoja wetu kufanya
kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Sheria zipo ili zitekelezwe” alisisitiza
Katibu Mkuu Mlawi.
Aidha, Katibu Mkuu huyo
amewataka watumishi hao kushirikiana kwa karibu na viongozi ili kuimarisha
umoja utakaoleta maarifa na ufanisi wa matokeo bora ya kiutendaji kwa manufaa
ya umma.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Nicholaus
William amewataka watumishi wote wizarani hapo pamoja Idara zote zilizopo
maeneo mengine kuzingatia nidhamu ya kutumia muda vizuri katika kuwatumikia
watu na umma kwa ujumla ili kujenga taifa lenye matokeo chanya ya kiutendaji na
hivyo kuleta maendeleo katika sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kama
inavyotarajiwa.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo
ya Michezo Bw. Yusuph Singo kwa niaba ya watumishi wote amesema kwamba wapo
tayari wakati wote kutoa ushirikiano kwa
viongozi wote bila kubagua na kwa kufanya kazi kwa kujituma ili kusukuma mbele
gurudumu la maendeleo ya Wizara.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment