NYALANDU SI MKWELI; OFISI YA SPIKA. - Mazengo360

Breaking

Wednesday, 1 November 2017

NYALANDU SI MKWELI; OFISI YA SPIKA.


IMEELEZWA taarifa za kudai kujiuzulu kwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) Mhe Lazaro Nyalandu sio za kweli kwani sio ofisi ya Spika wala Katibu Mkuu (CCM) aliyekwisha kupokea barua ya kujiuzulu kwake hadi leo.

 
Mhe Lazaro Nyalandu
Kulingana na taarifa rasmi iliyotolewa leo na ofisi ya Spika wa Bunge mjini Dodoma iliyoeleza kwamba imepata ufafanuzi toka Chama cha Mapinduzi kwamba, mchakato wa kumvua uanachama Mhe Nyalandu kwa kukiuka maadili ya chama ulikuwa ikiendelea na hivyo kujipotezea sifa za kuwa mbunge.

Ofisi ya Spika ilinukuu barua toka kwa Katibu Mkuu wa CCM iliyoandikwa October 30, kwenda kwa Spika wa Bunge (hata hivyo haikuonyeshwa) kwamba chama hicho kilishaanza kumchukulia hatua za kiudhibiti kutokana na matamshi yake ya kuupotosha umma kwa kauli zake za uwongo.

“Chama kilishaanza kumchukulia hatua za kiudhibiti na kinidhamu dhidi ya vitendo na kauli zake zisizoridhisha kinyume na misingi, falsa na itikadi ya Chama cha Mapinduzi” taarifa hiyo ya ofisi ya Bunge ilifafanua. 

Pia taarifa hiyo imenukuu sehemu ya kifungu cha sheria kwa mujibu wa Ibara ya 71 (l)(f) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba, 

“Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake cha ubunge iwapo litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo: (f) Iwapo Mbunge ataacha kuwa Mwanachama wa Chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa Mbunge” mwisho wa kunukuu. 

Kwa maana na kifungu hicho na ufafanuzi uliotolewa na CCM kuja kwa Spika wa Bunge ni wazi imemaanisha Mhe Nyalandu hakuwa mkweli alivyotangaza kujiuzulu kwa sababu alizozibainisha yeye bali yalikuwa matakwa ya chama chake cha CCM, hivyo alidanganya.

Juzi October 30, Mbunge huyo wa Singida Kaskazini (CCM) alinukuliwa kwenye mitandao ya kijamii na baadae kwenye vyombo takribani vyote vya habari akielezea kwamba ameamua kwa ridhaa yake kujivua nafasi zote katika chama, ikiwamo nafasi ya Ubunge Jimbo la Singida Kaskazini na pia kujiondoa uanachama wa CCM.

Mhe Lazaro Nyalandu ambaye amelitumikia Jimbo lake la Uchaguzi kwa kipindi kirefu kuanzia wakati wa Serekali ya awamu ya Nne iliyokuwa chini ya Rais Mstaafu Mhe Jakaya Mrisho Kikwete na kufanikiwa pia kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo uwaziri na pia kuwemo katika orodha ya walioomba ridhaa ya CCM kugombea Urais mwaka 2015.

Pia Mhe Nyalandu ambaye alijizolea heshima kubwa kwenye jamii wakati wa  kusaidia kufanikisha matibabu ya wanafunzi wahanga wa ajali ya gari ya Shule ya Lack Vincent ya jijini Arusha ambapo alitoa mchango mkubwa kufanikisha usafiri na matibabu ya wahanga watatu wa ajali hiyo kwa matibabu zaidi nchini Marekani.

Jitihada za kumpata msemaji mkuu wa CCM Humphrey Pole Pole ili kufafanua zaidi taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Spika hazikufanikiwa.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment