KATIBU
Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel amewaasa
watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendelea kufanya
kazi kwa bidii, kujituma na ubunifu mkubwa hata kama yeye amehamia wizara
nyingine.
Prof. Elisante ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akiwaaga watumishi wa wizara hiyo ambapo awali ndiye alikuwa anaiongoza kabla ya mabadiliko ya safu ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli hapojana Oktoba 26, 2017.
Prof Elisante amewaambia
kwamba “Tunapimwa kwa utendaji kazi hivyo, endelezeni utamaduni wa kuchapa kazi
kwa kujituma, kushirikiana, kupendana na kuwajali watumishi wote hasa wa ngazi
za chini” alisisitiza Prof. Elisante.
Aidha, amewashukuru
watumishi hao kwa ushirikiano waliompatia tangu alipoingia Wizarani hapo Aprili
01, 2012 akiwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, Naibu Katibu Mkuu na
baadae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambapo Idara ya Maendeleo ya Vijana kwa sasa
ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa
Maedeleo ya Utamaduni Bi. Lilly Beleko kwa niaba ya watumishi wengine amemhakikishia
Prof. Elisante kuwa wataendelea na uchapaji kazi kadiri alivyowaacha na kwa
ubunifu mkubwa kusukuma mbele shughuli za Wizara hiyo na taifa kwa ujumla ili
kuwaletea wananchi maendeleo kulingana na malengo ya Taifa iliyojiwekea.
Wakati huo huo Mkurugenzi
wa Sera na Mipango Petro Lyatuu amesema watamkumbuka Prof. Elisante kwa
utendaji wake wa kazi kwa kujali muda, kila mara na alikuwa akiwasisitiza
kutumia simu kimkakati kwa kupokea na kujibu simu ambapo kila mara alikuwa
akisisitiza “Simu zenu mziweke kimkakati wakati wote”.
Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo sasa inaongozwa na viongozi wapya ambapo Katibu Mkuu wake ni Bi.
Suzan Paul Mlawi na Naibu Katibu Mkuu akiwa Nicholaus B. William.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment