WAZAZI WAPAGAWA KWA MAADILI BORA KWA WASICHANA. - Mazengo360

Breaking

Thursday, 26 October 2017

WAZAZI WAPAGAWA KWA MAADILI BORA KWA WASICHANA.


WAZAZI na walezi wa wanafunzi wanaosomesha watoto wao wa kike katika shule za madhehebu ya dini wamepongeza uongozi wa shule hizo kwa kutilia zaidi mkazo katika nidhamu na maadili mema ambapo ndio msingi mkubwa wa waokujitambua na kufaulu vizuri katika mtihani.

 
Wazazi wakiipongeza meza kuu alikokaa mgeni rasmi Kaimu Mkurugenzi wa Elimu toka wizarani, Salim Salim (haonekani pichani). Kiongozi wa wazazi na walezi hao Madam Elieshi Mfangavo (gauni la bluu) akiwaongoza wazazi wenzake kuupongeza uongozi wa shule ya Mt Maria De'Matias ya mjini Dodoma hivi majuzi katika mahafali ya Tano ya shule hiyo ya wasichana. Anayetabasamu katikati mbele mezani ni Padre Mlezi wa Shule hiyo Fr Innocent Miku pamoja na viongozi wengine.
Wakibubujika kwa furaha baada ya kuwaona wasichana wa shule ya sekondari ya Mtakatifu Maria De’Matias inayomilikiwa na madhehebu ya Kanisa Katoliki mjini Dodoma wakati wa mahafali ya kadato cha Nne shuleni hapo siku ya jumamosi iliyopita October 21, wamesema wanaimani kubwa na shule hizo.

Mwakilishi wa wazazi na walezi hao alipopatiwa nafasi ya kuongea kwa niaba ya wengine Madam Elieshi Mfangavo kutoka Dar es Salaam alisema, hawawezi kujizuia kuonyesha furaha yao ilivyo kubwa kwani wamepagawa na kufarijika mno wanapowaona mabinti zao wakiwa katika hali ya nidhamu ya hali juu na pia kufanya vizuri katika masomo kulingana na ripoti za matokeo ya mitihani yao ya ndani na ile ya kimkoa na kitaifa.

 
Wazazi na walezi wakiendelea kuhamasika kwa furaha baada ya kuona watoto wao wakikaribia kuhitimu kidato cha Nne kwa viwango vizuri vya kitaaluma, maadili na malezi toka  shule ya sekondari ya wasichana ya Mt Maria De'Matia ya mjini Dodoma. Hapa ni siku ya mahafali ya Tano ya shule hiyo yaliyofanyika hivi majuzi shuleni hapo. Mgeni Rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia aliyewakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu (wizara) Bw Salim Salim.
Madam Mfangavo alisema “hakika hatuwezi kuizuia furaha yetu kwani Mungu ametufariji kwa mahangaiko makubwa ya kutafuta ada za kuwalipia watoto wetu katika mazingira magumu ya kiuchumi, lakini leo tunafurahia kwa ushindi huu ambapo Mungu ndiye aliyetuwezesha” alifafanua mzazi huyo.

Mzazi huyo Madam Mfangavo huku akinukuu maneno kutoka katika sehemu ya kitabu cha maandiko matakatifu cha Bibilia, Zaburi ya 126:2 kinachosema “ Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, Na ulimu wetu kelele za furaha” akimaanisha walivyofurahi kwa malezi bora ya mabinti zao na ndipo walipo hamasishana kuchangia mfuko maalum wa kuwapongeza waalimu na wanafanyakazi wote wa shule hiyo kama shukrani kwao.

 
Wanafunzi wa kidato cha Nne shule ya Sekondari ya wasichana ya Mt Maria De'Matias ya mjini Dodoma inayomilikiwa na madhehebu ya Kanisa Katoliki wakiwa katika mahafali yao ya Tano yaliyofanyika shuleni hapo mwishoni mwa juma lililopita. Mgeni Rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansina Taknolojia lakini akawakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu Bw Salim Salim (Hayupo pichani).
Shule ya sekondari ya Mt Maria De’Matias iliadhimisha mahafali yake ya tano hapo juzi jumamsi shuleni hapo, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe William Ole Nasha lakini akawakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu katika wizara hiyo Bw Salim Salim.

Akitoa hotuba yake ya pongezi kwa shule hiyo kwa niaba ya shule zote za madhehebu ya dini kwa kazi nzuri wanayofanya kuisaidia serekali kuwalea vizuri wanafunzi hususani wa kike, Mkurugenzi huyo pia alizishauri shule hizo za madhehebu ya dini zisijifungie zenyewe bali zishirikiane na shule zingine za umma na zile za binafsi kueneza mambo mazuri wanayofanya wao.

 
Mgeni Rasmi katika mahafali ya Tano ya shule ya sekondari ya wasichana ya Mt Maria De'Matias ambaye alimwakiliksha Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolijia Mhe William Ole Nasha , Kaimu Mkurugenzi wa Elimu wizara, Bw Salim Salim akimpongeza na kumtunuku cheti cha kuhitimu kidato cha Nne mmoja wa wanafunzi 63 wanaotarajia kuanzia mitihani yao Otober 30. Hapa Kaimu Mkurugenzi wa Elimu akimtunuku cheti mwanafunzi  Mariam Yohana Nchimbi (pichani) wakati wa mahafali hayo yaliyofanyika juzi jumamosi shuleni hapo. Wengine kutoka kushoto ni Sista Theresia Mwimba ambaye ni mshauri wa Shiriki la Masista wanaoendesha shule hiyo, akifuatiwa na Katibu wa Elimu Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Padre Revogatus Majuto akifuatiwa pia na Padre Mlezi wa shule hiyo Innocent Miku (kulia kwa mgeni rasmi) pamoja na wageni wengine katika mahafali hayo.
Alisema “wizara ya elimu kwa niaba ya serekali tunazipongeza sana shule za taasisi za dini kwa mchango mkubwa wa malezi na mafunzo ya kimaadili kwa wanafunzi wetu hususani wa kike, lakini tunawaomba msijifungie wenyewe bali shirikianeni na wengine ili nao waige kutoka kwenu” alisema Mkurugenzi huyo.

Alipokuwa akitoa neno la ukaribisho na pia kuelezea kwa ufupi sehemu ya mafanikio ya shule hiyo mbele ya hidhira hiyo,Mkuu wa shule hiyo Madam Lyela Lyimo alisema, uongozi wa shule hiyo inaishukuru sana serekali kwa kuandaa na kutekeleza vyema sera nzuri ya elimu ya mwaka 2014 ambapo shule yake ndio inayoifuata katika mfumo wa utoaji elimu.

Madam Lyimo alifafanua zaidi kwa kusema kwamba “sera nzuri ya elimu iliyopitishwa na serekali ndio msingi pekee kwetu, kutuwezesha kutoa elimu yenye kukidhi haja ya sasa kwa wazazi na walezi kwa wanafunzi hawa vinginevyo tusingeweza” alisema.

Akitoa historia fupi ya mafanikio ya shule hiyo, Madam Lyimo alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha Nne kitaifa mwaka jana 2016 shule ya Mtakatifu Maria De’Matias ilishika nafasi ya 56 kitaifa na ya pili kimkoa hapa Dodoma.

Madam Lyimo aliongeza pia kwamba, shule hiyo haina upungufu wowote wa rasilimali zikiwemo waalimu wa kutosha, vyumba vya madara na maabara, pamoja na viwanja vya michezo na vifaa vingine muhimu vya kufundishia.

Amewataka wazazi na walezi wenye mabinti zao katika shule hiyo wawe tayari kuwapokea watoto wao mara baada ya kumaliza mitihani yao ya mwisho ya kaidato cha Nne ambapo amesema wapo katika kiwango cha juu cha kitaaluma, kimaadili na nidhamu ya hali ya juu hivyo wasikubalike wabadilike.

Amemalizia kwamba, uongozi wa shule hiyo ina imani kubwa kwamba wote watafaulu mitihani yao ya kidato cha Nne kadiri walivyowaandaa na kusema zaidi kwamba wataendelea na masomo ya kidato cha tano mwakani pindi matokeo yatakapotoka hivyo wasiwaruhusu kujichanganya na makundi yatakayowafanya wasifikie azma hiyo njema katika maisha yao.

Shule hiyo ni ya wasichana pekee kuanzia chekechea hadi kidato cha sita na watakaofanya mitihani ya kidato cha Nne kuanzia October 30 wapo 63.

MWISHO. 

No comments:

Post a Comment