AKINA MAMA NCHINI WADAI HAKI KUMILIKI ARDHI. - Mazengo360

Thursday, 13 July 2017

AKINA MAMA NCHINI WADAI HAKI KUMILIKI ARDHI.

AKINA mama wanaojishughulisha na ukulima maeneo ya vijijini hapa nchini wamepaaza sauti zao kudai jamii itoe haki sawa ya kumiliki ardhi kama ilivyo kwa wanaume.

Action+Aid+3

Wakiwakilisha hoja yao hiyo mbele ya jukwaa la akina mama wanao jishughulisha na kilimo maeneo ya vijijini lililofanyika wilayani Chamwino mkoa wa Dodoma na kufadhiliwa na shirikala Action Aid (Tanzania), msemaji wa jukwaa hilo Bi Merea Surutwa alisema bado jamii inaendelea kukandamiza haki za akina mama maeneo ya vijijini.
Alisema, jamii katika maeneo ya vijijini hususani akina baba wakishirikiana na viongozi ngazi za vijiji pamoja na wa kimila na hata kata wanatumia  mfumo dume kupoka haki za wanawake.
Aliendelea kueleza katika taarifa yao maalum kwamba, wanawake ndio walezi wa familia na pia ndio wazalishaji wakubwa kupitia kilimo kwa kutumia ardhi wanayoimiliki waume zao kimila, lakini baada ya mazao kuvunwa, hawana haki ya kufaidi matunda ya kazi zao, taarifa hiyo ilieleza.
Alitoa mfano jinsi mwanamke wa kijijini anavyodhulumiwa haki ya kumiliki mali ikiwamo ardhi na kusema, jamii inachukulia jinsia ya kike kama bidhaa dhaifu ambayo haistahili kukaa meza moja na wanaume kupanga na kutumia matunda ya mazao ya shamba au nguvu za akina mama.
Taarifa iliendeleakueleza kwamba, mwanamke ndio tegemeo la familia kuanzia uzazi, malezi, kutafuta chakula na maji na pia kuhakikisha watoto wanakuwa na afya nzuri na wanaenda shuleni, huku pia wakijishughulisha na kazi za kilimo wakati waume zao wakikaa mabarabarani na kwenye vilabu vya pombe na maeneo minadani wakizurura bila kutoa msaada wowote kwao, taarifa hiyo ilieleza.
Jukwaa hilo la wanawake limetoa rai kwa jamii pamoja na viongozi wa kimila na kiutawala wakiwemo wa serikali za mitaa kuachana na mtindo huo wa kuwaona wanawake kama hawana thamani na kuwapatia haki.

Action+Aid+2

Nae mratibu wa mpango wa uwezeshaji gharama za uendeshaji katika sekta ya kilimo toka shirika la Action Aid (Tanzania), Bwana Jorum Wimmo alisema, jamii isipotambua hadhi na haki ya mwanamke na kutoa fursa sawa kwa wote, vita ya kuondoa umaskini katika jamii itakuwa vigumu kutekelezwa.
Mratibu huyo alisema pia kwamba, wenye dhamana ya kusimamia utoaji wa haki pamoja na kudhibiti matendo maovu yanayo mdhalilisha mwanamke, lazima yaachwe na kuhakikisha wanawasaidia wanawake ili nao wapate haki ya kumiliki mali ikiwamo ardhi, alisema.
Alitoa mfano wa sheria ya ya vijiji ya mwaka 1999 ibara ya tano inatoa haki katika mamlaka za vijiji nchini ambapo uwiano sawa wa mgawanyo wa mali baina ya wanawake na wanaume umeelezwa bayana.
Mratibu huyo wa Action Aid (Tanzania) alitoa wito kwa jamii pamoja na wanawake kwa ujumla kuhakikisha wanazielewa vizuri sheria na haki wanazopaswa kuwa nazo na kuhakikisha wanazipa ili zimkomboe mwanamke na kusaidia jamii itoke katika umaskini.

MWISHO.