WAAJIRI nchini
wametakiwa kuzingatia mgawanyo sahihi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma
ili kuwa na utendaji bora na wenye matokeo katika utumishi wa umma.
![]() |
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) akizungumza na viongozi na watumishi wa umma wa Halmashauri
ya Manispaa ya Ubungo (hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi katika Manispaa hiyo ili kupokea maoni,
ushauri na kusikiliza kero za watumishi wa umma leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah
J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Mhe.
Kairuki amesema mwajiri anapoomba kibali cha kuajiri watumishi ni vema
akazingatia mahitaji kulingana na majukumu yaliyopo ili kuondoa ziada ya watumishi wa umma wasio na kazi kuendana na
fani walizosomea kwa lengo la kuwa na utendaji mzuri.
“Ni
vizuri sana wakati tunaomba vibali vya kuajiri watumishi wa umma tukazingatia
mgawanyo sahihi wa rasilimaliwatu katika maeneo yetu kulingana na majukumu ya
watumishi tunaowahitaji badala ya kuomba watumishi wengi ambao wanasababisha
kuwa na ziada ambayo haitumika ipasavyo” Mhe. Kairuki amesema.
Waziri
Kairuki amesema katika vibali 10,184 vilivyotolewa hivi karibuni na Ofisi ya
Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa Mamlaka za Serikali
za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa, Wakala za Serikali, pamoja na Taasisi na
Mashirika ya Umma ili kujaza nafasi zilizoachwa na watumishi wa umma
waliobainika kughushi vyeti vya elimu, Halmashauri ya Manisapaa ya Ubungo
imetengewa jumla ya nafasi 140.
Aidha,
ameongeza kuwa, Halmashauri hiyo imetengewa jumla ya nafasi za ajira mpya 397
kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hivyo zitendewe haki kwa kuhakikisha watumishi
watakaoajiriwa wanafanya kazi kwa mujibu wa mpango uliopo.
Mhe.
Kairuki yuko katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es salaama kwa lengo la
kukutana na watumishi wa umma na kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto
zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi na kuleta
mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini ili kufikia malengo yaliyopangwa na
Serikali.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment