JAMII
maeneo ya vijijini bado inaendelea na mfumo dume wa kukandamiza wanawake
kijinsia na hata kuwanyima haki ya kufaidi matunda ya kazi za kilimo na ufugaji
na pia kunyimwa haki ya kumiliki ardhi kijamii kama walivyo wanaume.
![]() |
Wanawake kijiji cha Mloda (W) Chamwino, Dodoma. |
Hivi karibuni wilayani
Chamwino, mkoa wa Dodoma katika kijiji cha Mloda, Kata ya Mlowa Barabarani
kulifanyika kongamano la wanawake wanaojishughulisha na kilimo vijijini ambapo
walipaaza sauti zao kudai haki sawa kati ya wanawake na wanaume katika jamii.
Kongamano hilo
lililofadhiliwa na shirika la Action Aid hapa Tanzania, kupitia mradi wao wa kuwezesha
umma kifedha katika sekta ya kilimo, mratibu wa mradi huo Joram Wimmo
aliishauri jamii kuhakikisha wanawake wanapatiwa haki kutumia fursa ili kupiga
vita umaskini nchini.
Mratibu huyo alieleza
bayana kwamba, pamoja na sheria nyingi nzuri zinazolenga kumtetea na kulinda
haki za mgawanyo wa mali katika ngazi ya vijiji na kutaja sheria ya mamlaka ya
vijiji ya mwaka 1999, kipengele cha tano kinaeleza bayana haki ya jamii
kugawana sawa mali za jamii au familia baina ya wanawake na wanaume.
Ni jambo lililo dhahiri
kwamba wazalishaji wakubwa vijijini ni wanawake na ndio pia wanao shughulika
zaidi katika kilimo ili familia ijipatie chakula cha kutosha na kujiwekea akiba
kwa matumizi ya baade.
Pia wanawake ndio
wanaotunza na kuangalia watoto katika familia ikiwamo afya zao pamoja na
kuhakikisha watoto wanahudhuria shuleni pamoja na kuwakilisha katika vikao
namikutano ya wazazi vya shule kuhusu maendeleo ya watoto katika familia.
![]() |
Wakina mama wakiwasilisha ujumbe wao kwa jamii. |
Yapo malalamiko mengi yanayotolewa
na akina mama wanoaishi maeneo ya vijijini juu ya ukandamizaji kijinsia, ambapo
baada ya kuzalisha mali toka mashambani, akina mama hawapewe nafasi ya kupanga
namna ya kutumia matunda ya nguvu zao.
Mkaazi mmoja wa kijiji cha
Mloda, Kata hiyo ya Mlowa Barabarani Bi Mariam Chiseo, mwenye umri miaka 53
ameeleza kwa uchungu tabia za wanaume katika kijijini hicho wanavyo kandamiza
haki za akina mama na hata kutowaruhusu kufaidi matunda ya kazi zao.
Alieleza manyanyaso hayo
yakiwamo haki ya kutoshirikishwa katika kupanga matumizi ya mazao yanayovunwa
shambani mfano alizeti, mtama na hata mahindi pamoja na mifugo.
Aliendelea kueleza kwamba,
wanawake baada ya kuvuna na kuweka ghalani mazao hayo, baadae hushtukia mme
ameshaafikiana na wananunuzi au madalali wa ununuzi na kasha huja kuchukua mazao
hayo bilamakubaliano na mkwe na malipo husika hayawasilishwi kwa dhamira ya
manufaa ya familia.
Bi Mariam aliendelea
kueleza adha wanazozipata wanawake baada ya kuhoji, hupatiwa kipigo na
kufukuzwa nyumbani na waumme zao kisha hupotelea maeneo ya minadani kutumia
fedha hizo na marafiki pamoja na wanawake wa mitaani.
Ameiomba jamii pamoja na
mamlaka zinazohusika kusaidia kutatua tatizo hili kwani limeota mizizi na kuongeza,
“kamwe jamii haiwezi kutoka katika umaskini endapo hakutakua na hatua za makusudi
za kumkomboa mwanamke kutoka katika ukandamizaji huu” alieleza kwa uchungu.
![]() |
Bi Janet Nyamayahasi. |
Nae mwenyekiti wa Jukwaa la
wanawake hao Bi Janet Nyamayahasi ambae pia alishapata fursa ya kuwakilisha
umoja wa wanawake hao wanaojishughulisha na kilimo maeneo ya vijijini katika
vikao vya Umoja wa Afrika nchini Ethiopia, na pia kwenye Baraza la Umoja wa
Mataifa (UN) mjini New York Marekani, amesema yeye na wanawake wote
wamedhamiria kudai haki yao katika jamii.
Bi Janet aliendelea kutaja
malengo ya umoja huo ulioanzishwa mwakajana mwezi Octoba kwa kupanda milima ya
Uluguru na Kilmanjaro kupaaza sauti zao ilikupatiwa hakia ameeleza kunyimwa haki
ya kumilikishwa ardhi inayomilikiwa kimila na jamii ni kitovu cha kumkandamiza
mwanamke na kuchangiaumaskini.
Ameeleza lengo lao kuu ni
kuhakikisha wanapatiwa haki ya kumiliki ardhi pindi ifikapo mwaka 2025 na
kuomba msaada wa viongozi mbalimbali katika jamii wakiwamo wa mitaa, kiserikali
na wa kidini kusaidia kuelimisha umma ili wafikie lengo hilo.
Ametaja masahibu wanawake
wanayokutana nayo katika kunyimwa haki hiyo ikiwamo kumfanya mwanamke kama
bidha wakati wa kupanga mahari wanapoolewa.
“Wazee wa kimila hukaa
katika vikao vyao wenyewe na kukubaliana kiasi cha mahari kitakachobadilishwa na
mwanamke, na mara nyingi hua ni mifugo pamoja na fedha zinazopatikana baada ya
kupoka sehemu ya mazao yaliyozalishwa na mwanamke katika familia.”
Alifafanua Bi Janet
Nyamayahasi kwamba, Jambo hili lina athari kubwa na pia linachangia sana
umaskini katika jamii.
Mfano mwingine uliotolewa
na Bi Janet ni kuhusu ndoa za utotoni ambapo katika maeneo ya vijijini hususani
wilayani Chamwino mkoani Dodoma mtindo huu umeshamiri sana.
Aliendelea kueleza namna
wanafunzi wa jinsi ya kike wanapomaliza masomo ya shule za msingi na kukosa
nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari, wanavyoingia katika ndoa za utotoni
kwa tamaa tuu za wazazi wa kiume kupata mali kwa kubadilishana na motto wa
kike.
Amesema “mabinti wengi walio
chini ya umri wa miaka 18, wameozwa kwa waume japo sheria inawaruhusu tena kwa
waume wenye umri mkubwa na baade kuzalishwa watoto kwa tama tuu za mali, ambapo
ni kutanua umaskini katika jamii”, alisema kwa uchungu.
Tatizo jingine
linalowakandamiza wanawake na kusababisha jamii ibakie katika umaskini ni
unyanyasaji wa kingono ambapo wanawake wa rika zote wakiwamo wenye umri mkubwa
hubakwa na wenye fedha mfano wachuuzi wa mifugo na pia wafugaji.
Mabinti wa shule za msingi
na sekondari hudanganywa na makundi haya na kufanya vitendo vya ngono na baadae
kupata mimba na kufukuzwa mashuleni, kutokana tuu na umasikini unaowakabili
katika jamii.
Mwanamke mmoja (jina
limehifadhiwa) alitoa malalamiko yake mbele ya umati wa watu katika kongamano
hilo kwamba mnao mwaka jana alibakwa na mwanaume mmoja na ushahidi ukaonekana
lakini kutokana na nguvu ya fedha na ukandamiza wa mfumo dume, mashtaka
yaliyowasilshwa polisi yalibadilishwa toka ubakaji hadi shambulio la kawaida
lakimwili, hivyo sheria ikamtia hatiamlalamikiwa na kumtoza faini ya shilingi
laki tatu au kifungo miezi sita.
Ushuhuda mwingine wa
ukandamizaji ulitolewa na mkazi wa Kata ya Iringa Mvumi, wilayani Chamwino Bi Sona
Vumi ambae ni mjane, alisema aliolewa mwaka 1978 na mmewe kihalali na baade
mmewe aliugua na mwaka 2010 akafariki dunia.
Dada yake marehemu mmewe
(hakumtaja jina) alidiriki kumfukuza katika nyumba na shamba alilokuwa
akimiliki yeye na marehemu mmewe na kudai kwamba, hakuja katika familia yao na
mali.
Baade Bi Sona Vumi alitoa
taarifa katika baraza la Ardhi la Kata na akashinda shauri hilo na kuamuriwa
apatiwe haki na mali za marehemu mmewe, lakini mlalamikaji ambae ni wifi yake alienda
kukata rufaa katika mahakama ya wilaya kudai kwamba haki ya familia yao inanyang’anya
na mwanamke huyo.
![]() |
Diwani Mhe Salama Msigwa. |
Ili kuhakikisha haki za
akina mama zinatetewa, Diwani wa viti maalum (CCM) katika Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Chamwino Mhe Salama Msingwa amewataka akina mama wote
wanaonyanyaswa kijinsia, ikiwamo kubakwa na kudhulumiwa haki zao wafikishe
malalamiko yao kwenye baraza hilo ili wawasaidie.
Mhe Msigwa alifafanua
kwamba, endapo wanawake watabakia kuwa waoga kuchukua hatua dhidi ya
unyanyasaji, kwa kuhofia kutengwa na
jamii, wataendelea kunyanyasika na vyombo vilivyopo mfano Baraza la Madiwani
kushindwa kuwatetea
Ameeleza pia kwamba,
ameshangazwa na shuhuda za manyanyazo zilizotolewa katika kongamano hilo na
kusema, hazijafikishwa kwenye ngazi
rasmi za ufuatiliaji na utetezi hivyo, ametoa wito kwa wanawake wote kutoa
taarifa pindi wanapokutana na masahibu ya namna hiyo.
Kwa kuhitimisha makala hii ni
kwamba, wanawake ndio muhimili mkubwa wa uzalisha mali katika familia mijini na
vijijini.
Pia wanawake wanao mchango
mkubwa sana kubadilisha hali ya umaskini katika jamii endapo watapewa fursa na
hadhi sawa ya kupanga na kutumia mali zinazo zalishwa katika familia.
Vita vya kupambana na
umaskini hapa nchini itakuwa rahisi zaidi kama mwanamke watakombolewa katika
ukandamizaji na kupatiwa nafasi ya kumiliki mali ikiwamo ardhi kadiri sheria
inavyoelekeza, kwani ni waaminifu na wenye kujali zaidi ustawi wa familia.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment