WAAJIRI nchini wametakiwa
kufanya uhakiki wa kina wa vyeti vya elimu kwa ajira mpya zitakazotolewa ili
kuwa na watumishi wa umma wenye sifa zinazostahili katika utumishi wa umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb)
amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya
Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Kairuki amesema uhakiki wa kina
utasaidia sana kuepukana na kutojirudia tena kwa suala la watumishi wa umma
wanaoghushi vyeti.
“Jana tumetoa vibali vya ajira
10,184 kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa, Wakala za
Serikali, pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma ili kujaza nafasi zilizoachwa
na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu, hivyo napenda
niwasisitize sana waajiri wote kufanya uhakiki wa kina ili tusiwe tena na
watumishi wa umma wasiostahili katika orodha ya malipo” Mhe. Kairuki amesema.
Waziri Kairuki amesisitiza kuwa zoezi la
uhakiki ni endelevu ambapo lazima lifanyika pale mtumishi wa umma atakaporudi
katika kituo cha kazi kutoka masomoni, na watakaorejea katika utumishi wa
umma baada ya likizo bila malipo au sababu nyingine.
“Tunafanya hivi sio kwa nia mbaya, bali
tunataka tuwe na watumishi wanaostahili kuwepo katika utumishi wa umma kwa
sababu wanaoghushi wanaziba nafasi za wale wanaostahili kuwepo na wenye sifa
katika utumishi wa umma” Mhe. Kairuki aliongeza
Pia amewataka Waajiri kusafisha taarifa wa
watumishi wa umma mara kwa mara katika Mfumo Shirikishi wa Taarifa za
Kiutumishi na Mishahara (HCMIS).
“Kuna watumishi ambao muda wao wa kuwepo
kazini umemalizika (wamestaafu) lakini bado wanaendelea kuwepo, Mfumo wa HCMIS
sasa kila ifikapo saa 06:01 usiku utakuwa unawaondoa wale wote ambao muda wao
wa kuwepo kazini umefika lakini bado wanaendelea kuwepo kwenye Mfumo.
![]() |
Mstahiki
Meya Manispaa ya Kinondoni Mhe. Benjamini Sitta (kulia) akitoa neno la shukrani
kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) baada ya kupokea hoja za watumishi wa Umma
wa Wilaya ya Kinondoni leo Jijini Dar es Salaam. Pichani- Katikati ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) na kushoto ni
Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni Bw. Aron Kagurumjuli
Mhe, Kairuki yuko katika ziara ya kikazi
katika mkoa wa Dar es Salaam, ambapo leo ni siku yake ya nne aliyoitumia kukutana
na Watendaji na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni, baada ya kuzungumza na watumishi wa umma wa Temeke na
Mbagala.
Lengo la ziara ni kukutana na watumishi wa
umma na kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili katika
maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika
Utumishi.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment