WAKULIMA
wa Korosho nchini wamejipatia zaidi ya shilingi bilioni 800 kutokana na mauzo nje
ya nchi katika msimu uliopita wa mauzo zao hilo.
Takwimu hizo
zimetolewa leo na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. William Tate ole
Nasha wakati akifungua madhimisho ya siku ya Korosho iliyoadhimishwa kama
sehemu ya maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba)
yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu J.K Nyerere, Barabara ya Kilwa.
“Serikali imekuja na
utaratibu wa kuagiza mbolea kwa mkupuo na pia tutaanza kutoa mbolea kwa bei
elekezi. Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa tunawainua
wakulima wa Korosho na sekta ya kilimo kwa ujumla”, Aaisisitiza Ole Nasha.
Aliongeza kuwa tani
elfu 18 za mbolea aina ya salfa zitatolewa kwa wakulima bila malipo katika
msimu ujao wa korosho hali itakayosaidia kuwaongezea ari wakulima wa korosho
ambalo ndilo zao lililoingizia Taifa fedha nyingi zaidi za kigeni msimu
uliopita.
Katika kuwawekea wakulima
mazingira wezeshi Mhe. Ole Nasha alisema Serikali imeondoa tozo zaidi ya 140
zilizokuwa kero kwa wakulima hapa nchini ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukuza
kilimo kwa maendeleo ya viwanda na uzalishaji wa ajira.
“Kukua kwa kilimo kutasaidia
kuongeza ajira kwa vijana wetu wanaohitimu masomo katika vyuo mbalimbali ndio
maana tunaweka mkazo katika kukuza zao hili ambalo lina faida si za kibiashara
tu bali pia katika kujenga afya ikiwemo kupunguza lehemu mwilini, uzito na
kujenga kinga ya mwili”, alisisitiza Ole Nasha.
Kwa kuzingatia
umuhimu huo alitoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kula korosho kwani
kwa kufanya hivyo watakuwa wanakuza soko la ndani.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Kilimo) Mhandisi Methew Mtigumwe
amesema siku ya Korosho katika maonesho ya Sabasaba ni muhimu kwa kuwa
inawakutanisha wadau wa sekta hiyo kwa pamoja.
Pia aliwapongeza
wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo hali inayoonyesha
kuwa sasa kuna mageuzi makubwa katika sekta hiyo.
Bei ya Korosho katika
msimu uliopita kwa Kilogramu moja iliuzwa shilingi 4000/- hali inayoonesha kuwa
wananchi wakiunga mkono juhudi za Serikali kwa kuzalisha kwa wingi na kuongeza
thamani ya korosho wanazozalisha basi zao hilo linaweza kutoa mchango mkubwa
zaidi katika kujenga uchumi wa viwanda.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment