WANAHABARI SHINYANGA WAMTAKIA HERI RPC MULIRO. - Mazengo360

Tuesday, 18 July 2017

WANAHABARI SHINYANGA WAMTAKIA HERI RPC MULIRO.

LEO Jumanne Julai 18, 2017 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Saimon Sirro amefanya mabadiliko ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga.

IGP+SIRO
IGP SIMON SIRO.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, kufutuatia mabadiliko hayo ya kawaida, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Suzan Salome Kaganda amekuwa Mkuu wa kitengo cha Mafao na Fidia Makao Makuu ya Polisi, na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Murilo Jumanne Murilo aliyekuwa kamanda Polisi Mkoa wa Shinyanga.

ACP+Muliro+Jumanne.
ACP MULIRO JUMANNE.

Nafasi ya RPC Muliro imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Sylverius Haule, ambaye alikuwa Afisa Mnadhimu wa Polisi wa Mkoa wa Mara.
Mwenyekiti wa club ya waandishi wa Habari mkoani Shinyanga Kadama Malunde katika salamu zake kwa Kamanda Muliro alisema,
“Club ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (SPC), inamtakia majukumu mema RPC Muliro ambaye amekuwa nao mkoani Shinyanga kwa kipindi chote ambacho amekuwa akilitumikia vyema jeshi la polisi”.
SPC imesema pia kwamba, “tunamshukuru kwa ushirikiano wote aliokuwa akitupatia kwa muda muafaka pale tulipohitaji kulinganisha (to balance story) habari kwa upande wa pili ili kuihabarisha na kuielimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo kutokomeza na kufichua vitendo vya kihalifu ikiwemo mauaji ya watu wenye ualbino na vikongwe” salamu hizo zilieleza.
Akiwa mkoani Shinyanga, Muliro alikuwa anashirikiana bega kwa bega na waandishi wa habari na jamii kwa ujumla katika mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia, usalama barabarani na mambo mengine kadha wa kadha na kuufanya mkoa wa Shinyanga kuwa mahali salama pa kuishi.
SPC iliendelea kumpongeza Kamanda Muliro na kusema, hakuwa na tabia ya kupuuzia mambo anayoelezwa, ni mtu msikivu, siku zote amekuwa akitumia kauli ya “JIFUNZE KUSIKILIZA”.
Salamu hizo zilieleza pia kwamba, Kamanda Muliro mara kwa mara alikuwa akifika katika ofisi ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (SPC) siyo tu kikazi bali hata kubadilishana tu mawazo na kusalimiana.
SPC katika salamu zao wamesemapia kwamba, Muliro ni kiongozi ambaye alikubali mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, na pia ni mtumiaji mzuri wa mitandao ya Kijamii ikiwemo Whatsapp, na ili kuweka mawasiliano ya karibu kabisa na waandishi wa habari, Kamanda Muliro alikubali kujiunga katika Kundi la Whatsapp la waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ili kurahisisha utoaji wa taarifa za kipolisi mara tu matukio yanapotokea badala ya kujazana kwenye ofisi ya RPC.
Japo yapo mengi ya kusema kuhusu Kamanda Muliro, itoshe tu kusema kwamba sisi waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga hatukuona dosari kwa ndugu Muliro, tunamtakia kila la heri katika majukumu yake katika eneo lingine hapa nchini.
Tunamkaribisha sana Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Sylverius Haule kulitumikia jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga, na kumwahidi ushirikiano katikamajukumu yake, taarifa ya SPC ilimalizia hivyo.
MWISHO.