ACHENI KUIUMIZA FAMILIA YA LISSU: MBOWE. - Mazengo360

Breaking

Friday, 22 September 2017

ACHENI KUIUMIZA FAMILIA YA LISSU: MBOWE.

CHAMA cha upinzani cha CHADEMA leo kimeongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salam na kutoa wito kwa umma mzima kuacha kuendelea kuiumiza familia ya Tundu Lissu kwa malumbano yasiyo na msingi kuhusu afya ya Tundu Lissu.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mhe Freeman Mbowe akiongea na wanahabari.

Tundu Lissu, Mwanasheria wa CHADEMA na Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, lakini pia ni Mnajimu Mkuu wa kambi ya upinzania bungeni na Rais wa chama cha wanasheria nchini (TLS) alishambuliwa vikali na watu wasiojulikana na kudhuriwa vibaya mwili wake mnamo Septemba 07, akiwa mjini Dodoma.
Taarifa iliyoelezwa leo mbele ya waanahabari na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ambaye kwa muda wote huo alikuwa akiongoza kundi la wanaomuuguza Lissu hospitalini Nairobi Kenya, amesema si jambo zuri kwa umma kuendelea kukejeli shambulio la Tundu Lissu na kueleza zaidi kwamba ni kuendelea kuiumiza familia ya Lissu, hivyo waache mwenendo huo.
Hotuba hiyo ya Mhe Mbowe iliyochukua urefu wa muda wa saa moja na nusu ameeleza historia nzima ya tangu Lissu aliposhambuliwa na kundi la watu wasiojulikana mjini Dodoma akitokea bungeni na hadi sasa hakuna yeyote aliyekamatwa na kuutaka umm uache kupotosha taarifa za Lissu wasizozijua.
Mhe Mbowe ameuhakikishia umma kwamba, afya ya Tundu Lissu inaendelea kuimarika vizuri hospitalini Nairobi japo bado anakabiliwa na maumivu makali na kufafanua kwamba hofu ya Lissu kupoteza maisha kwa shambulio lile haipo tena na kuiomba jamii iendelee kumwombea na kumchangia gharama za matibabu yake.

Mke wa Mhe Tundu Lissu (kushoto) akiwa jijini Nairobi Kenya anakomuuguza mmewe. Wengine ni Mhe Edward Lowassa, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Mhe Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA na kiongozi wa timu inayomuuguza Lissu Nairobi (T-Shirt Nyekundu) na Dereva wa Tundu Lissu Adam Bakari (Kushoto).

Mbowe amesema gharama ya kumtibu Lissu tangu afikishwe hospitalini Nairobi Kenya hadi tarehe ya leo asubuhi Septemba 22, ni jumla ya fedha za Kenya kiasi cha Kshs 7.4 milioni ambapo ni sawa na fedha za kitanzania  Tshs 162.8 milioni ambapo ni gharama za matibabu peke yake akiwa hospitalini Nairobi, bila kujumuisha gharama za usafiri wa ndege wala zile za hospitali ya rufaa ya Dodoma siku ya shambulio.
Mbowe ambaye amesema kupona kwa Lissu kutokana na shambulio hilo ni miujiza ya Mungu, ametaja pia kiasi cha fedha zilizochangwa na watu mbalimbali hadi sasa na kusema waliochanga wengi ni watu wa kadi ya chini na wasio na kipato kikubwa.
Amebainisha kwamba kiasi cha fedha zilizochangwa hadi sasa ni Tshs 167.666 milioni na zilizopitia akauti ya benki ya CRDB tawi la Mbezi Beach ya jijini Dar es Salaam iliyotambulishwa na CHADEMA, ni kiasi cha Tshs 52 milioni na zile zilizopitia kwenye simu ya Vodacom kwa M-Peas ya Mhe Easter Matiko mbunge wa Tarime Mjini kuwa ni kiasi cha Tshs 24.2 milioni.
Zingine ni kutoka kwa wabunge wa CHADEMA jumla hadi sasa ni Tshs 48.465 milioni na toka bungeni kwa wabunge wote wakiwamo tena wa CHADEMA ni Tshs 43 milioni.
Mbowe amesema fedha zote zimeshatolewa na kufikishwa kwenye malipo hospitalini Nairobi isipokuwa zile za kutoka kwa wabunge kupitia ofisi ya bunge kiasi cha Tshs 43 milioni bado hazijawasilishwa au kutolewa hadi sasa.
Mbowe ambaye alionyesha kwa waandishi wa habari ankra ya benki ya CRDB na kuonyesha waliochangia matibabu ya Lissu, amesema ni kutoka kwa watu wa daraja la chini ambapo wengi wao wametoa mia tano,elfu moja na wengine elfu mbili na wa juu zaidi ni elfu tano, alibainisha Mbowe.
Aidha Mhe Mbowe aliendelea kueleza zaidi kwamba, kwa yeyote mwenye nia njema ya kuchangia matibabu ya Lissu anakaribishwa na CHADEMA, lakini akatoa wito kwa yeyote atakaye toa masharti ya kumchangia Lissu iwe kwa misingi ya kiitikadi au vinginevyo, hawapo tayari kuipokea.


Shangazi yake Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, Ninaa Sawa(kushoto) akiwa na mama mdogo wa Lissu, Bula Muro nyumbani kwa wazazi wa Mbunge huyo Mahambe, Ikungi  Singida, hivi karibuni.

Mbowe ameuhakikishia umma kwamba fedha zote zinazochangwa zipo salama na zinatumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na si vinginevyo na kuongeza kwamba kumbukumbu zote zipo kamili na tena kwa uwazi mkubwa, zikiwamo zile za matibabu ya Lissu hospitalini Nairobi na kusisitiza watu waache upotoshaji.
Hata hivyo Mbowe amesema, CHADEMA haijafungua kesi yeyote polisi hadi sasa kuhusu shambulio hili la Tundu Lissu na kusema zaidi kwamba, kipaumbele cha kwanza kwa sasa ni kuokoa maisha ya Tundu Lissu na sio vinginevyo.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu alipo dereva wa Tundu Lissu kwa sasa, Mbowe amesema yupo hospitalini Nairobi akipatiwa matibabu ya afya ya akili na kisaikolojia kwani nae alihathirika vibaya alivyo shuhudia hilokwa macho yake mwemyewe na akipona ataenda polisi kutoaushirikiano, alifafanua Mhe Mbowe.
Mbowe alimalizia hotuba yake kwa kuwataka watu wote wenye nia njema na Tundu Lissu waendelee kumwombea kwa Mungu ili apone haraka na akasema, kwa mapenzi ya Mungu atarudi kuendelea na majukumu yake, ambapo Mbowe amesema ni “mashine” ya kutetea haki za wanyonge.


Mbunge wa Singida Kaskazini -CCM Mhe Lazaro Nyalando (kushoto) akiwa jijini Nairobi katika hospitali anakotibiwa Tundu Lissu hivi karibuni.

Pia, amesisitiza Mhe Mbowe kwamba taarifa zozote zilizo rasmi kuhusu matibabu ya Lissu atakuwa akizitoa yeye kama mwenyekiti wa CHADEMA akiwa ama Dar es Salaam au Nairobi na kuwataka watu wasisikilize taarifa za kupotosha kutoka kwa vyanzo vingine, alitaadharisha Mbowe.
Kuhusu kumwamishia hospitali nyingi nga’ambo ikiwamo Ulaya na Amerika Mhe Mbowe ameeleza kwa sasa madaktari wanaomtibu jijini Nairobi wamesema haruhusiwa kuondolewa hospitalini wala kusafirishwa popote kwani ni hatari akipata mtikisiko wowote, hivyo ataendelea kutibiwa Nairobi Kenyahadi hapo baadae.


MWISHO. 

No comments:

Post a Comment