NI kama dhamira zimeanza kuwagusa viongozi wa dini na kuanza kuhimiza kuishi utu wema kadiri yasemavyo maandiko
katika vitabu vya dini vikiwemo Bibilia na Msaafu, ambapo kwa nyakati tofauti maaskofu wameanza kuelezea dhamiri zinavyowagusa kutokana na vitendo vinavyo endelea kwenye jamii yetu.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Ngara, Severin Niwemugizi. |
Baadhi ya viongozi wa dini akiwemo Askofu Mkuu Dkt Stephen Munga wa KKKT Jimbo la Kaskazini Mashariki la Tanga pamoja na sasa yule wa Kanisa Katoliki Jimbo la Ngara Severin Niwemugizi wameelezea jinsi wasivyofurahishwa na baadhi ya matendo yanayoendelea kwa sasa hapa nchini.
Pia Baraza la Maaskofu Katoliki nchini
(TEC) na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Ubungo Dar es Salaam, Josephat Gwajima
walishatoa misimamo yao juu ya matendo ya kikatili yaliyoanza kuibuka nchini.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Ngara,
Severin Niwemugizi amesema yuko tayari kuitwa mchochezi endapo kundi la
watetezi wa haki za binadamu watachukuliwa kama wachochezi.
Askofu Niwemugiza amesema yeye kama
kiongozi wa dini anaongozwa na maadili, haki na ukweli hivyo hajali namna
wengine watakavyomchukulia.
Akifungua mkutano wa asasi za kiraia
ulio lenga kujadili kuhusu Katiba Mpya leo Jumatano, Askofu Niwemugizi amesema
imefika wakati nchi inahitaji kuwa na dira nzuri.
Amesema hakuna mtetezi wa haki za
binadamu anayetaka nchi iingie kwenye machafuko kwani wote lengo lao ni
kuchochea maendeleo, amani na utulivu.
Askofu Niwemugizi amesema kuanza
kutokea kwa matukio ya kuteka watoto, vifo katika mazingira ya kutatanisha na
ongezeko la watu wasiojulikana ni ishara mbaya.
"Hizi sio dalili nzuri kwa
Taifa lenye afya njema. Ni vielelezo vyenye dira mbaya. Imefika wakati tukae
kama Taifa tukubaliane kuwa tunataka dira njema ambayo ni Katiba."
Amesema anatambua jitihada
anazofanya Rais John Magufuli katika kupambana na ufisadi na kutaka rasilimali
ziwanufaishe wanyonge lakini ni muhimu juhudi hizo zilindwe na Katiba nzuri.
"Rais anafanya mengi mazuri na
alipoanza kila mmoja aliona dalili za matumaini lakini juhudi hizo zinaweza
zisiwe endelevu kama hakuna ulinzi wa Katiba,”
"Tunahitaji Katiba tena Katiba
nzuri ambayo haitaruhusu kuchezewa na yeyote kwa maslahi au matakwa yake
binafsi."
Amesema, "Namshauri Rais
achunguze kwa makini yatakayozungumzwa kwenye mkutano huu, ayaone kuwa
yana nia njema na ayafanyie kazi.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment