Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa
pongezi za dhati kwa Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking kutokana
na utendaji kazi wake uliotukuka katika kudumisha ushirikiano baina ya Tanzania
na China hususani katika nyanja za masuala ya habari, utamaduni, sanaa na
michezo.
Pongezi hizo amezitoa hivi karibuni wakati wa hafla ya kumuaga balozi huyo iliyowakutanisha baadhi ya Viongozi wa Chama cha Ushirikiano wa Rafiki wa Tanzania na China wakiwemo Waandishi wa habari.
Moja
ya mambo makubwa muhimu yaliyofanyika chini wakati wa kipindi cha Balozi Lu
Youking ni tukio la utiaji saini mwezi Machi mwaka huu ambapo Serikali ya
Tanzania na China zilitiliana saini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiutamaduni wa
Miaka mitatu ambao utawapa fursa vijana 200 kutoka Tanzania kila mwaka kwenda
China kwa ajili ya kupata mafunzo katika nyanja mbalimbali za habari, sanaa na
utamaduni.
Dkt
Mwakyembe alisema, "Balozi Lu Youking umetuachia zawadi kubwa sana sisi
Wanahabari wa Tanzania, sasa hivi mimi na wenzangiu Wizarani tunakamilisha
utaratibu wa utekelezaji wa Mkataba huu ili tuanze kuutekeleza mapema
iwezekenavyo", alifafanua.
Aliongeza
kuwa, Balozi Lu Youking hivi karibuni ameshirikiana na Balozi wa Tanzania
nchini China, Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki katika kuhakikisha kwamba Waandishi wa
habari 10 kutoka Tanzania wanaondoka mwezi ujao kuelekea nchini China kwa ajili
ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya habari.
Kwa upande wake Balozi Lu Youking alisema kwamba, urafiki kati ya Tanzania na China umekuwa wa afya na imara zaidi ya nusu karne akikumbushia kuwa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake aliwahi kusema kwamba, Tanzania ina marafiki wengi, lakini China ni zaidi ndiyo maana Rais wa China, Mhe. Xi Jinping alichagua Tanzania kuwa kituo chake cha kwanza Afrika wakati wa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuwa mkuu wa nchi.
Aliongeza
kuwa, kila mwaka zaidi ya Wanafunzi 700 kutoka Tanzania huenda China kwa ajili
ya masomo zaidi na kutokana na hilo, matokeo ya ushirikiano wa China na
Tanzania umekuwa wa manufaa katika maeneo yote ya uchumi wa Tanzania na
maendeleo ya jamii na kwa kila maisha ya Mtanzania.
“Uhusiano wa China na Tanzania umetoa mwongozo kwa Ushirikiano wa Kusini na Kusini yaani South-South Cooperation, hivyo kutokana na maendeleo ya ushirikiano huu katika uwezo wa uzalishaji kati ya China na Tanzania na mpango wa Ukanda mmoja njia moja, tunaamini ushirikiano huu utakuwa na matunda zaidi”, alisema Balozi Youking.
Urafiki
baina ya Tanzania na China ulianzishwa na Waasisi Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha
China, Bw. Mao
Tse-Tung (Mao Zedong) ambapo uhusiano baina wa nchi hizi mbili kwa sasa umekuwa
kwa kasi na kuleta maendeleo baina ya pande zote mbili.
MWISHO
No comments:
Post a Comment