SERIKALI
kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inatarajia kuanzisha Taasisi
ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) ili kuweza kuzalisha wataalam wa ngazi ya kati
wenye ubobezi katika sekta ya ujenzi.
Hayo yalisemwa na
Mkurugenzi wa Barabara Mhandisi John Ngowi wakati wa kongamano la pili la
kujadili hatua mbalimbali zilizofikiwa juu ya uanzishwaji wa Taasisi hiyo jana
jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Ngowi amesema kuwa
kuanzishwa kwa taasisi hiyo hapa nchini kutawezesha kuondoa pengo la uwiano
baina ya wahandisi na kada za chini kama mafundi sanifu na mafundi mchundo
ambao ndio wasimamizi wa karibu wakati kazi za ujenzi zinapotekelezwa.
“Mpango mkakati wa Wizara
yetu pamoja na mambo mengine, unahusisha uimarishwaji wa sera zinazohusu ujenzi
kwa kujenga mazingira wezeshi,mafunzo ya ufundi na matumizi ya teknolojia
mkakati ambao utawezesha kutatua changamoto za umahiri na ubobezi inayokabili
sekta ya ujenzi,” alisisitiza Mhandisi Ngowi.
Mkurugenzi wa Barabara toka Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi John Ngowi (wanne kutoka kushoto) akiwa katika
picha ya pamoja na wadau wa sekta ya ujenzi mara baada ya kufungua kongamano la
pili la majadiliano kuhusu uanzishwaji wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi
(ICoT) leo Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mhandisi Ngowi ameongeza
kuwa uanzishwaji wa taasisi hiyo itakuwa
chachu ya kufikia azma ya serikali ya awamu ya tano katika kuelekea uchumi wa
kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kuongeza rasilimali watu ambao ni muhimu
katika usanifu, usimamizi, ujenzi na ukarabati wa miundombinu.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Kampuni ya EcomResearch ambayo ni mshauri wa uanzishwaji wa ICoT Profesa Godwin Mjema amesema kuwa mipango ya uanzishwaji wake umefikia hatua nzuri ambapo
umeshirikisha wadau mbalimbali ili kujadili Kozi na mitaala itakayotumika
kufundishia.
“Sisi kazi yetu ni kushauri
tume hatua tuliyofikia, ili wadau wajadili na kukubaliana na yale tuliyoandaa,
wakikubaliana na sisi tutakabidhi kwa wizara ambao ndio wamiliki na wao
watawasilisha Baraza la Taifa Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa hatua za usajili,”.
alisema Profesa Mjema.
Kuanzishwa kwa taasisi hii
kunatokana na kuendelea kupanuka kwa pengo kati ya waandisi na kada za chini
hali iliyotokana na vyuo vingi vya ufundi kupandishwa hadhi kuwa vyuo vikuu
katika miaka ya 1990 bila kuanzishwa vyuo vingine vya ngazi ya kati hasa vya
fani ya ujenzi.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment