WAKUTANA ARUSHA KUJADILI MALEZI YA WATOTO. - Mazengo360

Monday, 4 September 2017

WAKUTANA ARUSHA KUJADILI MALEZI YA WATOTO.

NCHI 13 za bara la Afrika na wanataaluma mbalimbali wanakutana katika mkutano wa siku tatu mkoani Arusha kubadilisha uzoefu wa kitaaluma kuhusu uzingatiaji wa huduma ya kisaikolojia katika malezi  na makuzi bora ya watoto na vijana.

Pix+1-1
Naibu Waziri wa Afya maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto  Mhe. Dkt Hamis Kigwangalla akihutubia washiriki kutoka nchi 13 za Afrika wanaoshiriki mkutano wa masuala ya huduma ya kisaikolojia katika maelezi na makuzi ya watoto na vijana unaofanyika ukumbi wa AICC mjini Arusha.

Akifungua mkutano huo katika ukumbi wa AICC Arusha, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Jinsia na Watoto Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla ameeleza kuwa mkutano huo utatoa fursa kwa Serikali, asasi za kiraia, na wanataaluma kutumia fursa hiyo kubadilishana uzoefu, kujenga uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa huduma ya kisaikolojia katika malezi na makuzi ya watoto na vijana katika nchi za bara la Afrika.
 Ameongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa kuzingatia masuala ya huduma ya kisaikojia katika maendeleo ya mtoto kama yanavyosisitizwa katika utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki na Ustawi wa Mtoto (CRC) na Mkataba wa Nchi za Kiafrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC).
“Mikataba hiyo ya Kimataifa na Kikanda, inazitaka nchi wananchama wa umoja huo kuwa na mifumo thabiti ya ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo mbalimbali vya ukatili na unyanyasaji ili kuhakikisha utoaji wa haki  na uhuru kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi husika” alisema Dkt Kigwangalla.

Pix+5-1
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Mhe. Dkt Hamis Kigwangalla akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Serikali, Wakurugenzi watendaji wa Shirika la REPSSI na wajumbe wa Bodi ya shirika hilo, AICC Arusha.  

Dkt.Kigwangalla amewakumbusha washiriki wa mkutano kuwa, ulinzi wa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili unakuza kwa kiwango kikubwa maendeleo ya  kisaikolojia kwa mtoto na vijana kwa kutekeleza mipango mbalimbali inayotoa kipaumbele katika kuwekeza kwa watoto.
Aidha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga amewahakikishia REPSSI kushirikiana na Wizara katika utekelezaji wa shughuli zao ili kufikia malengo ya utoaji wa elimu na huduma ya kisaikolojia kwa wadau wanaotoa huduma za ulinzi wa watoto.
“Tuna waahidi ushirikiano wadau wetu katika masuala ya kumsaidia mtoto hasa mtoto wa Kiafrika na Kitanzania katika masuala ya utoaji huduma za kisaikolojia” alisema Bibi Sihaba

Pix+3
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la REPPSI Bibi Noreen Huni akitoa maelezo kuhusu shughuli za Shirika la REPSSI katika kipindi cha mika 15 tangu kuanzishwa kwake wakati wa mkutano wa huduma ya kisaikolojia katika malezi na makuzi ya watoto unaofanyika Arusha, Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la REPSSI Bibi Noreen Huni amewapongeza watoto 76 kutoka nchi hizo 13 za Afrika kwa kushiriki mkutano huo  wakati REPSSI inaadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake.
“Shirika letu limebaini kuwa ushughulikiaji wa mahitaji ya kisaikolijia kwa watoto una nafasi kubwa kwa Afrka kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030; hususani lengo namba 3, 4, 5, na 16” alisema Bibi Noren.
Mkutano wa Kimataifa wa Malezi na mkuzi kwa wavulana,wasichana na vijana wa mwaka 2017 umeshirikisha wadau kutoka nchi 32 Duniani na unafanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 04 mpaka 06 2017 ukiwa na kauli mbiu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wasichana na Wavulana na Vijana wote kwa ujumla”.

MWISHO.