MENEJA wa Arsenal
Arsene Wenger amesema “alisita” kusaini mkataba mpya msimu uliopita akiwa na
mashaka iwapo kama bado “ana uwezo wa kuongoza klabu hiyo”.
![]() |
Kocha wa Arsenal Arsene Wenger akiwa na wenzake katika benchi la Ufundi. |
Wenger alikubali kusaini mkataba wa
miaka miwili mwezi Mei, mwezi mmoja tu kabla ya mkataba wake kumalizika.
Akizungumza na kituo cha televisheni
cha Ufaransa, katika kipindi cha michezo cha Telefoot, alisema kulikuwa na
“sababu binafsi” zilizomfanya kuchelewa kusaini mkataba mpya katika klabu hiyo
ambayo ameiongoza kwa miaka 21.
Lakini aliongeza kusema: “Nimekuwepo
pale kwa muda mrefu, na najiuliza kama naweza kuipeleka timu katika ngazi
nyingine?”
Arsenal walimaliza katika nafasi ya
tano katika ligi kuu msimu uliopita- ikiwa ni mara ya kwanza kumaliza nje ya
nne bora tangu Wenger alipojiunga na Arsenal mwaka 1996. Hata hivyo Arsenal
walishinda Kombe la FA kwa kuwafunga Chelsea.
“Nimekuwepo Arsenal kwa miaka mingi
na msimu uliopita tulisumbuka sana,” amesema Mfaransa huyo, 67.
“Mwaka huu tulishinda mchezo wetu wa
kwanza, hatukuwa vizuri kwenye mechi ya pili, halafu tukaonesha kiwango kibovu.
“Lakini sasa tunahitaji kuibuka
tena, na kama kawaida, wakati wa matatizo unahitaji kushinda mchezo ujao.”
Wenger aliulizwa kuhusu dau la
Thomas Lemar, 21, wa Monaco katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili.
Ada ya uhamisho ya pauni milioni 90
iliripotiwa kuafikiwa lakini Wenger alisema mchezaji huyo “aliamua kubakia
Monaco”.
Alipoulizwa iwapo anapanga kurejea
tena Monaco kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa, Wenger alisema:
“Ndio. Nadhani ni mchezaji wa kiwango cha juu.”
Pia alisema alitaka kumsajili Kylian
Mbappe, ambaye amejiunga na Paris Saint-Germain kwa mkopo na ambao hatimaye
utakuwa uhamisho wa pauni milioni 165.7(euro milioni 180) msimu ujao.
“Milioni 180 ni kiasi kikubwa kidogo
kwetu,” alisema Wenger, ambaye amemuelezea Mbappe, 18, kama “Pele
anayechipukia”.
(Taarifa na picha kwa hisani ya BBC).
MWISHO.
No comments:
Post a Comment