SHONZA KUSIMAMIA ZAIDI MAADILI. - Mazengo360

Breaking

Tuesday, 17 October 2017

SHONZA KUSIMAMIA ZAIDI MAADILI.

NAIBU WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Juliana Shonza leo amepokelewa wizarani kwake mjini Dodoma na kuahidi kusimamia kwa karibu maadili bora katika jamii ili kujenga jamii yenye kuheshimiana na kujenga taifa lenye umoja na lililo imara.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ofisi za Wizara leo mjini Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe.

Mhe. Shonza ambaye anaaminika ndiye waziri kijana kupita wote katika baraza la sasa la mawaziri, ameyasema hayo leo mjini Dodoma wakati alipopokelewa na viongozi waandamizi wa wizara hiyo akiwamo Waziri mwenye dhamana Dkt. Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri anayeondoka pamoja na viongozi wengine wa Wizara na  watumishi wengine.

Naibu Waziri alisema “Wizara hii ni muhimu sana kwa kuwa inajenga taswira ya taifa kupitia sekta zake ambazo ni Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo hivyo ni muhimu sana tunashirikiana kwa pamoja ili kuwatumikia wananchi na akaongeza kuwa nguzo pekee ya kutuvusha ni kuzingatia maadili” alifafanua Mhe Shonza.

Pia Mhe. Shonza ameahidi kutoa ushirikiana mkubwa kwa watendaji wote wa wizara, pamoja na wadau wengine wote pamoja na wananchi kwa ujumla katika kusimamia maadili ya Mtanzania ambapo aliongeza kwamba ni muhimu sana kwa sasa.


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa Naibu Waziri wizara hiyo Mhe. Anastazia Wambura leo mjini Dodoma.

Naye aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo Anastazia Wambura amempongeza Naibu Waziri Shonza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na amemshukuru pia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kumuamini alipomteau katika baraza lake la kwanza.

Alizungumzia zaidi utendaji kazi ambapo Mhe. Wambura ameufananisha utumishi wa umma na chombo cha usafiri ambapo abiria hushuka kituoni anapofika na dereva kuendelea na safari, hivyo amemtakia mafanikio mema Mhe Shonza.

Aidha Mhe Wambura alisemweleza Mhe Shonza kwamba, anamkabidhi kijiti cha uongozi nae aendeleze alipoishia, huku akimpongeza kwani ni heshima kubwa kwao wote Mhe Rais ameonyesha hivo kumtakia utumishi mzuri pamoja na viongozi wengine wa wizara.


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (wa pili kushoto) akiongea na baadhi ya viongozi wa Wizara akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kushoto) mara baada ya kuwasili ofisini mjini Dodoma. Wa kwanza kulia ni aliyekuwa Naibu Waziri wizara hiyo Mhe. Anastazia Wambura.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amemuahidi Naibu Waziri Shonza ushirikiano wa hali na mali katika kuwahudumia wananchi kupitia sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.


MWISHO.

No comments:

Post a Comment