JPM : "SIKUJA SEREKALINI KUTAFUTA MCHUMBA". - Mazengo360

Thursday, 7 September 2017

JPM : "SIKUJA SEREKALINI KUTAFUTA MCHUMBA".

RAIS Dkt John Magufuli amesema “Sikuja Serekalini kutafuta mchumba, bali kuwatumikia watanzania na hivyo sipo tayari kuona mali za watanzania zikiporwa kwa kumwonea mtu aibu kwa kumlinda”

Ikulu+Leo+3
RAIS Dkt John Pombe Magufuli akipitia kwa ufupi ripoti ya ukaguzi ya madini ya Tanzanate na Almasi iliyowasilishwa kwake na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa leo Ikulu jijini Dar.
Rais ameseam, "Sikuja kutafuta mchumba serekalini, hivyo sitamwonea aibu yeyote anayefuja mali ya Umma".

Rais Dkt Magufuli leo amekuja kivingine kabisa wakati wa kupokea ripoti mbili maalum za kamati ya bunge juu ya uchunguzi wa madini ya Tanzanate na Almasi iliyowasilishwa kwake na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Ikulu jijini Dar.
Rais kupitia hotuba yake aliyoitoa na kurushwa moja kwa moja na vyombe mbalimbali vya habari kwenda kwa watanzania wote, leo ameonyesha kuwa mpole na mwenye subira zaidi katika hotuba yake lakini yenye ujumbe mzuri,mpana kwa watanzania.

Rais aliyasema hayo leo baada ya kukabidhiwa ripoti hizombili na Mhe Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Ikulu jijini Dar nakuonyesha kusikitishwa mno na baadhi ya wateule wake kutajwa katika kashfa  hii ambapo yeye ameeleza wazi kwamba ni kukosa uzalendo kwa taifa letu kwa kiwango kikubwa.

Ripoti hizo mbili ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na bunge baada ya Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai kuunda kamati maalum ili kuchunguza mwenendo wa uchimbaji madini ya Tanzanate na Almasi hapa nchini.

Tunaungana watanzania wote wenye nia njema kwa Taifa letu la Tanzania kumpongeza Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa namna alivyokuja mbele ya umma hivileo na kuwaelezea jinsi Taifa linavyofilisiwa na baadhi ya watanzania waliokabidhiwa na wengine amewateua yeye kusimamia rasilimali zetu watanzania.

Ikulu+Leo+2
RAIS Dkt John Pombe Magufuli akipokea vitabu vya ripoti ya ukaguzi ya madini ya Tanzanate na Almasi iliofanywa na kamati maalum ya Bunge iliyoundwa na Spika wa Bunge la Tanzania Mhe Job Ndugai na kuwasilishwa kwake na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ripoti hiyo imewataja baadhi ya viongozi wateule waandamizi wa serekali kwa uzembe mkubwa uliyoisababishia Taifa hasara kubwa, hivyo Mhe Rais kuwataka wote waliotajwa kujiuzulu nyadhifa zao kupisha uchunguzi wa TAKUKURU.

Rais leo katika hotuba yake ameonekana mpole, mtulivu lakini mwenye kubeba hisia kubwa ya kutaka kuchukua hatua za kurekebisha mwenendo wa watendaji serekalini.

Rais amekuja tofauti kabisa na wakati ule alipopokea ripoti ya makontena ya mchanga wa makinikia  wa ACACIA.

Rais amesikitishwa zaidi hususani aliposikia hata baadhi ya waliotajwa katika ripoti hizi mbili wapo wateule wake aliowaamini sana ambapo ndio sababu haswa ya yeye kuonyesha subira ile kubwa hivi leo.

Baadhi ya waliotajwa katika ripoti hizo ni pamoja na Waziri katika ofisi yake anaye shughulikia na usimamizi wa Tawala za Mikoa na Serekali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe George Simbachawene, ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe-CCM, toka Mkoani wa Dodoma.

Mteule mwingine ambaye ametajwa katika ripoti hizi kwa sasa ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe Edwin Ngonyani.

Viongozi hawa wawili waandamizi ambao ni wateule wa Rais ni wazi wamemuaibisha mno Mhe Rais na hadi kumfanya awe mpole na mwenye umakini wa kuzungumza katika hotuba yake.

Ikulu+Leo
RAIS Dkt John Pombe Magufuli akipokea ripoti ya uchunguzi ya madini ya Tanzanate na Almasi toka kwa Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia katikati ni Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai na Mwenyekiti wa kamati iliyofanya uchunguzi huo Mhe Musa Azzan Zungu (Mb) akishuhudia kushoto.
Mhe Rais Dkt Magufuli anaonekana usoni kuwa mpole na mwenye simanzi kubwa kwa haya yanayotokea.

Rais amewaomba radhi sana watanzania kwa vitendo vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wanaokabidhiwa wajibu wa kusimamia rasilimali za watanzania na kuwataka wale wote waliotajwa katika ripoti hizo kuachia nafasi zao ili kupisha uchunguzi ambao Idara ya TAKUKURU imekabidhiwa kuianza rasmi.
Jambo la pili ambalo Rais Dkt Magufuli ameonyesha utofauti kabisa wakati huu ni hatua yake ya kuwapongeza waziwazi wabunge wa upinzania walioshirikishwa katika kamati hiyo ya bunge.

Rais amesikakia akisema wazi kwamba, “watanzania tuache tofauti zetu za kivyama au kiitikadi tuangalie uzalendo kwa nchi yetu”, huku akimtaja kwa jina mbunge wa upinzani wa Jimbo la Momba kupitia CHADEMA Mhe Silinde.

Katika hili Rais Dkt Magufuli amedhihirisha wazi kwamba yeye ni baba wa wote, bila kuchagua mwana-CCM au mpinzani ila ni Rais wa watu wote.
Hakika hapa Rais ameonyesha uzalendo wa hali ya juu hususani kwa kukubali kwamba sote ni watanzania na kila mtu anaweza kulitumikia taifa lake kikamilifu bila kujaliitikadi zake kivyama endapo watapatiwa nafasi ya kufanya hivyo.

Hapo jana wakati wa kamati ikikabidhi ripoti zake mbili kwa Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai na baadae pia kuzikabidhi kwa Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa, kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na mbunge wa Hai Mhe Freeman Mbowe (CHADEMA) alimpongeza Spika kwa hekima kubwa ya kiuongozi aliyotumia na kuwashirikisha wabunge wa vyama vyote bila kubagua, jambo ambalo ni zuri na wakatekeleza jukumu hilo vizuri, alielezea Mhe Mbowe katika hotuba yake.

Aidha, ni imani ya watanzania wote kwamba muhimili wa mahakama nao utatekeleza wajibu wake hapo baadae wakati TAKUKURU itakapokamilisha wajibu wake wa uchunguzi kama mihimili hii miwili ya serekali na bunge walivyofanya pia.

Jambo la tatu ambalo Mhe Rais Dkt Magufuli amelionyesha ni kule kutoa wito kwa chama chake cha CCM ambapo yeye ndiye mwenyekiti wake kwamba sekretarieti husika iwasilishe ripoti juu ya viongozi wana-CCM wanaotajwatajwa katika kashfa za kila mara ilichama kiwashughulikie.

Ikulu+Mpya
Ikulu jijini Dar es Salaam

Rais amesema chama kinazo taratibu zake za kuwaadhibu wanaojihusisha katika kashfa kadha wa kadhaa. Nyakati zingine si kawaida sana kuwaeleza wana-CCM wenzake mbele ya umma bali hufanyika vikao vya ndani ya chama na ndiko wanakoelezana haya.
Hii inadhihirisha wazi Mhe Rais ameanza kuchoka kuwavumilia wana-CCM wenzake hadi kulazimika kuitisha chama kilete ripoti hiyona kujadiliwa kama dondoo maalum ya mkutano.

Jambo la nne alilolionyesha  Mhe Rais  ni kule kukiri wazi kwamba wateule wake wanamwangusha na wajumbe wa kamati hiyo ya bunge imemwonyesha imani kubwa kwamba wanaweza kumsaidia vizuri katika uongozi wa nchi kwani wameonyesha uzalendo wa hali ya juu sana. 

Rais amesema wazi kwamba, baada ya kupokea ripoti ya kamati hii ya bunge, sasa amepata wasaa wa kuangalia upya timu ya watendaji wake watakaomsaidia kuendesha serekali, huenda akalazimika kufumua baraza zima lamawaziri na kuliunda upya na kuwateua baadhi ya wabunge kumsaidia.
Ni wazi Mhe Rais ameonekana kufarijika sana kwa kazi nzuri iliyofanywa na Spika wa bunge kwa kushirikiana na wabunge wote.

Rais pia ameonyesha kuridhika sana na ripoti mbili hizi zilivyoandaliwa kwani zilipitia mtindo wa mikataba ya madini, inavyosafirishwa nje ya nchi na mapato au kodi inayolipwa serekalini.

Hongera sana Rais pamoja na Waziri Mkuu wako. Hongera pia Mhe Spika na wabunge wote kwa uzalendo mkubwa.
Watanzania sasa tuipe serekali nafasi ili kazi iliyoelekezwa kwa TAKUKURU ifanyike vizuri na kuikamilisha mapema kama alivyo elekeza Mhe Rais Magufuli.


“MUNGU IBARIKI TANZANIA”.