WATANZANIA wametakiwa
kuuenzi na kuulinda utamaduni wao kupitia Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika
Mashariki (JAMAFEST) ili waweze kuleta maendeleo katika masuala ya ujasiriamali
na utalii nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole-Gabriel akihutubia
Tamasha la Kiutamaduni na Sanaa kwa nchi za Afrika Mashariki maarufu kama
JAMAFEST, Kampala Uganda.
|
Pia kuufanya uwe bidhaa yao
katika kuutambulisha utanzania wao hususani katika masuala ya vyakula, mavazi
ya asili, nyumba za asili, utamaduni usioshikika pamoja na lugha ya Kiswahili.
Kauli hiyo imetolewa leo
Mjini Kampala, Uganda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na
Michezo, Prof. Elisante Ole-Gabriel katika Tamasha la Kiutamaduni na Sanaa kwa
nchi za Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST.
Prof. Elisante ameeleza
kuwa, Utamaduni ndiyo silaha pekee inayoweza kuwaweka watu pamoja ambapo
amesisitiza kuwa, Watanzania hawanabudi kuulinda utamaduni wao ili uweze
kuwaletea maendeleo huku akigusia suala la lugha ya Kiswahili, matumizi ya
vyakula vya asili, matumizi ya mavazi ya asili pamoja na nyumba za asili kuwa
vitu hivyo vina uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo nchini.
Akizungumzia kuhusu
matumizi ya lugha ya Kiswahili alisema kwamba, lugha hiyo imekuwa ni ya 10 kati
ya lugha zinazozungumzwa Duniani na inazungumzwa na watu zaidi ya nchi 50
katika Bara la Afrika.
Ameongeza kuwa, lugha ya
Kiswahili inaweza kutumika kama bidhaa ambapo juhudi za kutosha kupitia Wizara
yake zinafanywa katika kuhakikisha kuwa lugha hiyo inatumika zaidi kwa ufasaha
na kubidhaishwa ulimwenguni kote.
“Kupitia Baraza la
Kiswahili la Taifa (BAKITA), tunahakikisha kwamba Kiswahili kinabidhaishwa
ndiyo maana hivi karibuni Waziri wetu Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
alizindua Kamusi Kuu ya Kiswahili Bungeni Mjini Dodoma, kwahiyo tukio lile
limekuwa chachu ya pekee na limeongeza uzito mkubwa katika lugha ya Kiswahili”,
alisema Prof. Elisante.
Amebainisha kuwa, Tamasha la JAMAFEST litasaidia kuondosha tofauti mbalimbali baina ya nchi za Afrika Mashariki na litasaidia kuzifanya nchi hizo kuwa kitu kimoja kwakuwa zitakuwa zinashikamana na lugha ya Kiswahili ambayo kwa kiasi kikubwa inatumika katika nchi hizo.
“Tukiweka utamaduni wetu
ukawa unaingiliana basi tutafika muda itabidi tuanze kusahihisha zaidi kufafana
kwetu na sio kutofautiana kwetu na hakika hakuna atakayebaguliwa kwani umoja
wetu huo utaleta faida kubwa katika masuala ya uchumi wa viwanda kwasababu soko
litakuwa kubwa baina ya nchi zetu za Afrika Mashariki”, alisema Prof. Elisante.
Kwa upande wake Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Bibi Joyce Fissoo amesema kwamba, Tamasha la
JAMAFEST limeleta fursa mbalimbali katika masuala ya utamaduni kama vile
vivutio vya kiutamaduni, vivutio vya kiasili, ambapo Tanzania imepata fursa ya
kuwa na mada tano zinazozungumzia masuala ya hifadhi, masuala ya filamu
hususani mchango wa filamu katika uchumi wa Taifa, masuala ya filamu na muziki,
masuala ya Sheria na taratibu zinazosimamia sekta za utamaduni na ubunifu.
Amefafanua kuwa, mada
ambazo zimetolewa na Viongozi mbalimbali toka Tanzania zimeakisi masuala muhimu
ya utamaduni, umuhimu wa kuuhifadhi utamaduni, umuhimu wa sekta za ubunifu
zikiwemo na filamu.
“Tamasha la JAMAFEST
linasaidia kuimarisha utangamano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, linatanua wigo wa masoko ambapo bidhaa mbalimbali
zinapatikana toka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, pia linatangaza vivutio
vya nchi wanachama, lakini pia linatangaza rasilimali za nchi wanachama ambapo
kwa upande wa Tanzania tumeweka mambo ya kipekee jambo ambalo limewavutia watu
mbalimbali kuja kuona vitu vyetu”, alisema Bibi Fissoo.
Katika Tamasha hilo,
Tanzania imewakilishwa na wadau wapatao 247 ambapo kati yao 71 wanatoka
Tanzania Visiwani (Zanzibar) ambapo baadhi ya vikundi vya ngoma na bendi vimehudhuria
pia kwa upande wa Tanzania Bara kuna vikundi mbalimbali vya Sanaa toka Taasisi
ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBA) pamoja na vinginevyo ambavyo vimehudhuria katika
Tamasha hilo.
“JAMAFEST ni fursa kwa nchi
wanachama kwakuwa nje ya utamaduni, ubunifu, na mitindo tamasha hili linatoa
fursa ya mapato kwahiyo kwa kiasi kikubwa tumechangia kwa namna moja au
nyingine kuongezeka kwa mapato kwa moja ya nchi wanachama ambayo ni Uganda,
lakini tunatarajia na sisi kwa tamasha lijalo kufanyika kwetu hapo baadaye
itakapotangazwa”, aliongeza Bibi. Fissoo.
Kaulimbiu katika Tamasha
hilo ambalo lilianza mwaka 2013 nchini Rwanda linasema ‘Utamaduni na Ubunifu,
Kiini cha Ajira na Umoja’. Tamasha hilo linahusisha mambo mengi baina ya nchi
wanachama hususani masuala ya vivutio vya utamaduni wa asili.
MWISHO
No comments:
Post a Comment