KANISA
Katoliki limewaomba watanzania kumwombea Rais Dkt John Pombe
Magufuli ili atimize dhamira yake ya kuwapigania wanyonge na kuondoa
umaskini nchini kwani kazi hiyo ni ngumu na yenye vikwazo vingi.
Wito huo umetolewa leo mjini
Dodoma na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaia
wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada maalumu ya Misa ya kutoa daraja la
Upadrisho iliyofanyika katika kanisa kuu la Jimbo la Mt Paulo wa Msalaba.
Askofu Mkuu Kinyaia alimwagia
sifa Rais Dkt John Magufuli kwa utendaji wake kazi mzuri na mahiri hususani kwa
kutetea haki za wanyonge wa Taifa hili na kueleza kwamba, anafurahishwa sana na
utendaji wake.
Alisema, “ninawaomba
waumini wote na watanzania kwa ujumla kumwombea kwa Mungu Rais Dkt John
Magufuli ili aweze kutekeleza azma yake njema ya kuwatetea wanyonge na pia
Mungu amwepushe na maadui wabaya,”alifafanua Askofu Kinyaia.
Katika Ibada hiyo ambapo Askofu Kinyaia alitoa daraja la Ushemasi na Upadre kwa watawa wawili hivi leo, aliwataka pia vijana waache kukaa vijiweni na badala yake wafanye kazi kwa bidii na kutumia muda wa ujana wao vizuri ili wajipatie maendeleo na waepuke uvivu.
Akitoa mfano wa utendaji wa
Rais Dkt Magufuli, Askofu Kinyaia amewataka vijana kubadilika na kumuunga mkono
Rais katika jitihada zake za kuhimiza maendeleo na kuongeza kwamba, hakuna mafanikio
yanayokuja kwa maneno matupu hivyo wasikie na kumuunga mkono Rais Magufuli.
Pia amewahusia wafuasi wa
kanisa hilo hapa nchini kutekeleza wito wa kufanya kazi kila mtu kwa bidii na
ubunifu mkubwa kwani ndio mpango wa mungu kwa wanadamu, na pia ndicho Rais
anachohimiza, alieleza Askofu Kinyaia.
Amwahusia watendaji katika
kada za ualimu na afya kwamba, kazi zao zinahitaji zaidi wito hivyo waombe kwa
mungu awajalie karama ya upendo, uvumilivu na moyo wa kuwasaidia wengine ili
wanyonge wapate faraja wanapohitaji huduma zao.
Nae Mkuu wa Shirika la
Mapadre wa Mateso ya Yesu hapa nchini Padre Greogory Olomy amemshukuru Askofu
Mkuu Beatus Kinyaia kwa moyo wake wa upendo na matashi mema kwa watu wote wa
taifa hili, na kuahidi kuendelea kushirikiana nae pamoja na jamii kwa ujumla kuhimiza
mambo mema, ili jamii ipate amani.
Pia Mkuu huyo wa Shirika
ametoa wito kwa padre na shemasi ambapo
wote wapochini ya shirika hilo kwamba waende kuwasaidia vijana katika jamii
kufuata mifano mema kwa kufanya kazi ili wabadilike.
Askofu Mkuu Kinyaia ametoa
daraja la Ushemasi kwa Frateri Stephano Omondi ambae ni raia tokea nchini Kenya
na pia daraja la Upadrisho kwa Padre mpya Erastus Kamugisha wote wa Shirika la
Kitume la Mateso ya Yesu hivi leo mjini Dodoma.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment